Majibu ya DED Kahama yashindwa kumridhisha Rais Magufuli

Muktasari:

Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri mji Kahama mkoa wa Shinyanga nchini Tanzania, Anderson Nsumba amejikuta katika wakati mgumu baada ya kutakiwa na Rais John Magufuli kujibu hoja na maswali ya wananchi.

Mwanza. Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri mji Kahama mkoa wa Shinyanga nchini Tanzania, Anderson Nsumba amekuwa kiongozi wa kwanza wa umma kukumbana na joto la ziara ya Rais John Magufuli baada ya kushindwa kutoa majibu ya hoja na maswali ya wananchi.

Nsumba ameonja joto hilo leo Jumatano Novemba 27, 2019, baada ya Rais Magufuli kumwita kujibu hoja na kero za wananchi wakati wa mikutano yake ya hadhara inayorushwa moja kwa moja na vituo vya runinga.

Kwa mara ya kwanza, majibu ya mtendaji huyo wa halmashauri kuhusu utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa kituo cha mabasi cha mjini Kahama yalipata upinzani kutoka kwa Rais Magufuli baada ya kusema fedha za utekelezaji zitapatikana kupitia mkopo wa benki.

Jibu la mkurugenzi huyo lilitokana na hoja ya mmoja wa wananchi kuhusu kukosekana kwa stendi ya kisasa ya mabasi kwenye mji wa Kahama wenye shughuli nyingi za kiuchumi kutokana na biashara na uchimbaji wa madini ya dhahabu.

Katika jibu lake akasema Halmashauri ya Mji Kahama yenye bajeti ya jumla ya zaidi ya Sh37 bilioni anatarajia kutekeleza mradi wa ujenzi wa stendi kupitia fedha za mkopo kutoka Benki ya TIB.

Jibu hilo halikumridhisha mkuu huyo wa nchi na kuhoji inawezekanaje halmashauri yenye mapato ya zaidi ya Sh37 bilioni ishindwe kutekeleza mradi wa ujenzi wa stendi kwa fedha zake za ndani hadi ichukue mkopo wenye riba benki.

“Kwanini msitumie fedha zenu hadi mkakope benki na mlipe kwa riba? Hebu kakope uone,” amesema Rais Magufuli akihitimisha suala hilo

Katika mkutano mwingine, Nsumba amejikuta majibu yake yakikosa kumridhisha Rais Magufuli kuhusu ujenzi wa shule ya msingi katika moja ya kata za Wilaya ya Kahama.