Makarani wa vituo vya kura wasisitizwa kuwa weledi, waadilifu

Baadhi ya Makarani wasaidizi katika Jimbo LA Mbeya mjini wakila kiapo kabla ya kupata mafunzo ya namna ya usaidizi kwa wapigakura Oktoba 28 mwaka huu.

Muktasari:

Wapewa mafunzo wakitakiwa kuwapa kipaumbele wajawazito, wenye ulemavu, wazee na wenye mahitaji maalumu.

Mbeya. Mafunzo ya makarani waongozaji wa vituo vya kupigia kura yamefanyika katika jimbo la Mbeya mjini ambapo wametakiwa kurahisisha shughuli ya upigaji kura

Katika jimbo hilo makarani 3,040 kati ya 10,000 waliojitokeza kuomba nafasi hiyo wamepatiwa mafunzo hayo.

Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Mbeya Mjini, Amede Ng'wanidako amefungua mafunzo hayo leo Oktoba 25 kwa mujibu wa kanuni za uchaguzi 2020.

Ng'wanidako amewataka makarani hao kuendesha zoezi hilo kwa utashi na uadilifu mkubwa kwa kuwapokea na kuwaongoza wananchi kwenye vituo vya kupigia kura.

"Mkawe chachu ya kurahisisha zoezi hilo kwa wasimamizi wa uchaguzi na mtoe kipaumbele kwa makundi ya wajawazito, wenye ulemavu, wazee na wengine wenye mahitaji maalumu," amesema Ng'wanidako.

Ng 'wanidako amesema kuwa weledi na uadilifu utaleta matokeo chanya ya kufanikisha mwanzo wa zoezi mpaka wakati wa kuhesabu  ikiwa ni pamoja na kuwataka wananchi wakipiga kura  kuondoka kwenye vituo.

Karani mwongozaji kutoka Kata ya Sinde jijini  hapa, Regina Joel amesema kutokana na maelekezo waliyopewa na msimamizi wa uchaguzi shughuli hiyo itaendeshwa kwa ufanisi mkubwa sambamba na kuyasaidia makundi maalumu.

Amesema pia watazingatia mwongozo wa kuhamasisha wapigakura katika vituo kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni katika maeneo yaliyotengwa ili kukabiliana na magonjwa yanayoambukizwa kwa njia ya mikono, hususan Covid 19.