VIDEO: Makonda aagiza ujenzi soko la Magomeni kukamilika Desemba 2019

LIVE: ZIARA YA RC MAKONDA KATIKA MIRADI YA MAENDELEO DAR

Muktasari:

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ameagiza ujenzi wa  soko la Magomeni jijini Dar es Salaam kukamilika Desemba 2019 badala ya mwaka 2020.

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ameagiza ujenzi wa  soko la Magomeni jijini Dar es Salaam kukamilika Desemba 2019 badala ya mwaka 2020.
Pia, ameagiza kuitishwa kwa kikao cha wafanyabiashara baada ya kuibuka kwa malalamiko kwamba ujenzi unafanyika bila ushirikishwaji.
Ametoa kauli hiyo leo Jumanne Oktoba Mosi, 2019 wakati akikagua miradi ya manispaa ya Kinondoni, kubainisha kuwa soko hilo litakalogharimu Sh8. 5 bilioni lilipaswa kukabidhiwa mwaka 2020 lakini linatakiwa kukabidhiwa Desemba, 2019 sambamba na ujenzi wa jengo la machinjio ya Vingunguti.
"Kabla ya Ijumaa muwe mmekaa kikao mjadili lengo la soko ilikuwa ghorofa tatu lakini hizi ni mbili na niliagiza vizimba visipungue sasa hivi watu wanalalamika vidogo," amesema Makonda.
Awali baadhi ya wafanyabiashara walilalamika kutoshirikishwa katika ujenzi wa soko hilo na hivyo kushindwa kutoa ushauri.
Ali Juma, mfanyabiashara soko la Magomeni amesema walitamani soko hilo liwe la jumla badala ya rejareja kama ulivyo sasa.
Mwenyekiti wa soko hilo, Subiman Mtalazaki amesema kama wafanyabiashara watakaa katika ghorofa itakuwa vigumu kwao kufanya biashara hoja iliyomfanya Makonda asisitize kuwa vitu vinavyovutia wateja vikae juu.
Mshauri mwelekezi wa jengo hilo,  Henry Moleka amesema ujenzi huo utakamilika Desemba, 2019.