Makonda aanza safari ya kuwapigania wajane

Wednesday August 28 2019
makondapic

Dar es Salaam. Kilio cha muda mrefu cha wajane wanaodhulumiwa mali huenda kikapatiwa ufumbuzi wa kudumu baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam nchini Tanzania, Paul Makonda kuingilia kati.

Makonda akiongoza timu ya wanasheria wa mkoa huo wanatarajia kupeleka mapendekezo kwa Waziri wa Katiba na Sheria (Balozi Agustine Mahiga) ili kufanyia marekebisho sheria ya mirathi.

Akizungumza leo Jumatano Agosti 28,2019 Makonda amesema timu yake ya wanasheria imefanya utafiti kubaini chanzo cha kuwepo malalamiko mengi ya wajane ndipo ilipobaini kuna udhaifu kwenye sheria.

Mkuu huyo wa mkoa amesema kongamano lilifanyika Aprili 2019 lililowakutanisha wajane ndilo liliwasukuma kufanya utafiti huo kubaini chanzo cha malalamiko ya kundi hilo.

Amesema udhaifu huo uliopo kwenye sheria ndio umekuwa ukitumika kuwadhulumu wajane kwa kuwanyima thamani ya kusimamia mali walizochuma na wenza wao.

“Sheria ya mirathi tunayotumia ni ya mwaka 1865 hii tumerithi kutoka India kwanza imekuwepo kwa muda mrefu na ina mapungufu mengi,” amesema

Advertisement

Miongoni mwa upungufu huo ni kutompa uhalali mwanamke kusimamia mali zilizoachwa na mumewe, kesi za mirathi kusikilizwa kwa muda mrefu pamoja na sheria kuwa kimya kuhusu wanawake kutolewa kwenye nyumba zao baada ya waume kufariki.

“Mapendekezo tunayopeleka kwenye sheria hiyo tunataka mke awe sehemu ya msimamizi wa mali za marehemu mumewe hadi pale mahakama itakapotoa uamuzi kuhusu mirathi,” amesema Makonda

Aprili 4, 2019 Makonda alikutana na wajane waliojitokeza kwa wingi katika ukumbi wa Mlimani City ambapo walitoa matatizo mbalimbali huku yeye (Makonda) akiahidi kutafuta ufumbuzi wa changamoto walizozibainisha.


Advertisement