Makonda akagua ujenzi barabara Moroko –Mwenge akionya wanaotiririsha maji taka

Monday November 04 2019
Makonda pic

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amewaonya wananchi wenye tabia ya kutiririsha maji taka na kutupa taka katika mifereji ya maji ya mvua.

Amesema kufanya hivyo kunasababisha uchafuzi wa mazingira na kuongeza uwezekano wa kutokea kwa mafuriko.

Makonda ameyasema hayo leo Jumatatu Novemba 4, 2019 alipokuwa anakagua maendeleo ya ujenzi wa Barabara ya Moroko hadi Mwenge sambamba na ujenzi wa mitaro ya kutolea maji ya mvua katika maeneo ya Mwananyamala Bwawani.

Barabara hiyo ya Mwenge - Moroko yenye urefu wa Kilomita 4.3, inajengwa kwa fedha zilizotolewa na Serikali ya watu wa Japan Sh77.3 bilioni.

Akizungumza baada ya kukagua miradi hiyo, Makonda amesema ujenzi wa mifereji hiyo umelenga kuondoa adha ya kujaa kwa maji katika makazi ya watu iliyokuwa ikitokea miaka ya nyuma.

“Rais wa Tanzania John Magufuli anayafanya haya yote kwa ajili ya manufaa ya Watanzania wote, sasa siyo nyie mtumie mitaro hii kutiririsha maji yenu ya chooni, haijatengenezwa kwa ajili ya kazi hiyo na wala siyo kwa ajili ya kutupa takataka, maji haya yote yataelekezwa moja kwa moja baharini,” amesema Makonda.

Advertisement

Akizungumzia upanuzi wa barabara, Mkuu huyo wa mkoa amesema baada ya kukamilika kwa njia nyingine nne mpya, barabara zilizopo sasa katika eneo la Mwenge - Morocco zitatumika kwa ajili ya magari ya mwendokasi.

“Lakini pia kuanzia Bamaga hadi Shekilango, mkandarasi yupo barabara inajengwa kwa njia nne ambao utaweza kuondoa adha ya msongamano wa magari kwa wananchi.”

“Haya yote yanajengwa kwa jitihada za Rais wa Tanzania, John Magufuli anayetaka maendeleo amuunge mkono asiyetaka aache,” amesema Makonda.

Mmoja wa wakazi wa eneo la Mwananyamala Bwawani, Issa Abdallah ameshukuru juhudi za ujenzi wa mifereji unao endelea huku akibainisha kuwa itawaondolea adha ya kujaa kwa maji katika maeneo yao kipindi cha mvua.

“Mvua zilikuwa zikinyesha eneo hili, maji yanajaa ni rahisi kupata magonjwa ya miripuko kwa sababu watu hutumia fursa hiyo pia kutiririsha maji machafu ya nyumbani kwao,” amesema Abdallah.

Advertisement