VIDEO: Makonda amjibu Waziri Jafo kiaina

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda (wa pili kutoka kushoto) akimsikiliza Meya wa Manispaa ya Ilala, Omar Kumbilamoto (kulia) wakati alipofanya ziara katika mradi wa ujenzi wa machinjio ya kisasa Vingunguti leo. Picha na Anthony Siame

Muktasari:

  • Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda atatumia kipindi cha Septemba na Oktoba 2019 kusimamia ipasavyo utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika mkuo huo ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Rais wa Tanzania, John Magufuli.

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam (RC) nchini Tanzania,  Paul Makonda amewaomba mawaziri wa Serikali ya Tanzania kumvumilia ili akamilishe maelekezo yaliyotolewa na Rais John Magufuli.

Makonda ametoa kauli hiyo ikiwa imepita siku moja tangu Waziri wa Tamisemi, Seleman Jafo kumpa mkuu huyo wa mkoa siku 14 kuhakikisha ameitisha kikao cha taasisi tatu ili kupata mwafaka wa ujenzi wa soko la kisasa la Kisutu.

Taasisi hizo ni Manispaa ya Ilala, ofisi ya Wakala wa Barabara Tanzania- Dar es Salaam na Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT) ambazo zimeshindwa kuafikiana katika ujenzi wa soko hilo.

Waziri Jafo alitoa maagizo hayo jana Jumamosi Septemba 28, 2019 alipotembelea mradi huo wa soko la Kisutu akisema, “Ndani ya wiki mbili (Makonda) aitishe kikao na Manispaa ya Ilala, Meneja wa Tanroad mkoa wa Dar na BRT kwa sababu yupo ndani ya ofisi yangu, nipate taarifa haraka.”

 

Hata hivyo, leo Jumapili Septemba 29, 2019 Makonda wakati akikagua mradi wa machinjio ya Vingunguti amesema ameridhishwa na kasi yake kutokana na mkarandasi kutekeleza majukumu yake usiku na mchana.

"Mawaziri wanivumilie kidogo, mwezi huu (wa Septemba) na wa 10 baada ya hapo waje kufanya ziara katika mkoa huu, nataka kila kitu kikae sawa.”

“Nafuatilia maelekezo yaliyotolewa na Rais Magufuli na yale yaliyojiri katika mkutano wangu na watendaji wa mkoa huu," amesema Makonda.

Maelekezo ambayo anayasema ya Rais Magufuli ni yale aliyoyatoa hivi karibuni aliposema haridhiki na utekelezaji wa miradi mbalimbali katika mkoa huo ikiwemo ya machinjio ya Vigunguti pamoja na maboresho ya ufukwe wa Coco akihoji mkoa huo kama kuna viongozi.