Makonda amtaka mratibu Tarura kuweka kambi Tamisemi

Muktasari:

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam amtaka Mratibu wa Tarura katika mkoa wa Dar es Salaam kupiga kambi Tamisemi mpaka atakapopata fedha za fidia ya wakazi wa Makongo.



Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam nchini Tanzania, Paul Makonda amemtaka Mratibu wa Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (Tarura)  mkoani humo, George Tarimo kwenda kupiga kambi ofisi za Tamisemi mpaka atakapopata majibu ya malipo ya fidia ya fedha za  ujenzi wa barabara ya Makongo.

Zaidi ya Sh4 bilioni zinapaswa kulipwa fidia ili kupisha ujenzi wa barabara inayoanzia Chuo cha Ardhi, Makongo mpaka Goba jijini Dar es Salaam.

Akizungumza baada ya kupokea tathmini ya hali ya barabara ya wilaya ya Kinondoni leo Jumatatu Februari 24, 2020, Makonda amemtaka mratibu wa Tarura kuanzia kesho Jumanne asifike ofisini isipokua aende Tamisemi akatafute majibu ya fidia hiyo.

"Kesho ondoka, nisikuone mkoani mpaka utakapokuja na pesa za Makongo, mnakaa kusubiri majibu labda hawajaona barua yenu kaweke kambi mpaka upate hela,"  amesema Makonda.

Awali, Tarimo amesema bado hawajapewa majibu ya malipo ya fidia hiyo licha ya kuwa waliwasilisha maombi.

"Fidia tuliwasilisha hatujapata majibu," amesema Tarimo.

Akiwasilisha taarifa ya hali ya barabara za wilaya ya Kinondoni, Mbunge wa Kinondoni (CCM), Maulid Mtulia amesema ili mkandarasi aendelee na ujenzi wa barabara hiyo lazima fidia ilipwe.

Amesema ujenzi wa barabara hiyo unagharimu Sh8.2 bilioni.