VIDEO: Makonda ataka barabara za juu Ubungo kuitwa Magufuli Interchange

Muktasari:

  • Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amependekeza barabara za juu katika makutano ya barabara ya Morogoro, Mandela na Sam Nujoma Ubungo jijini Dar es Salaam kuitwa Magufuli Interchange.

Dar es Salaam.  Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amependekeza barabara za juu katika makutano ya barabara ya Morogoro, Mandela na Sam Nujoma Ubungo jijini Dar es Salaam kuitwa Magufuli Interchange.

Zaidi ya Watanzania 800 wameajiriwa katika mradi wa ujenzi wa barabara hiyo iliyofikia asilimia 60.

Akizungumza leo katika ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo mkoani humo leo Jumatatu Oktoba 7, 2019,  Makonda amesema jina hilo linaakisi jitihada za Rais wa Tanzania, John Magufuli kuharakisha maendeleo.

“Hili ndilo lango la kuingilia Dar es Salaam mradi huu ni ishara kuwa Rais Magufuli ameweka alama na ni utambulisho kuwa yupo anafanya kazi, ningependekeza iitwe jina lake,” amesema Makonda.

Amesema kwa sababu barabara hizo zimejengwa ili kupunguza foleni, taa zitakazowekwa lazima ziendane na  msongamano wa magari kwa nyakati husika hasa asubuhi na jioni.

“Asubuhi watu wengi wanaingia mjini na jioni wanatoka mjini kurudi nyumbani kwa hiyo hayo muhimu yazingatiwe,” amesema kiongozi huyo wa mkoa wa Dar es Salaam.

Meneja uzalishaji wa mradi huo, Yan Chuang amesema mbali na ajira zaidi ya 800, vifaa vingi vinavyotumika kwenye ujenzi vinazalishwa  katika viwanda vya ndani ya nchi.

“Wafanyakazi wanalipwa vizuri kila mwezi, kazi inafanyika bila wasiwasi na Juni 2020 ujenzi wa barabara hizo utakamilika ,” amesema Chuang.

Kwa upande wake msimamizi wa mradi huo,  Eric Chatwin amesema mpaka sasa mradi huo umekamilika kwa asilimia 60.

Amesema barabara hizo ndilo suluhisho la kudumu la foleni kwenye eneo hilo.