Makonda aunda kamati kusimamia ujenzi Coco Beach, machinjio Vingunguti

Tuesday September 17 2019
pic makonda

Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ameunda  kamati maalumu  kusimamia utekelezaji wa miradi ya kimkakati katika mkoa huo ambayo itahusisha wataalamu mbalimbali wakiwemo maofisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

Hatua hiyo imekuja siku moja baada ya Rais wa Tanzania, John Magufuli kumwagiza Makonda kuhakikisha miradi ya ujenzi wa Coco Beach na machinjio ya Vingunguti yenye thamani ya  Sh26 bilioni inakamilika kwa wakati.

Makonda ametoa kauli hiyo leo Jumanne Septemba 17, 2019 katika hafla ya utoaji udhamini kwa wanafunzi wa kike 100 wanaosoma masomo ya Sayansi lakini wazazi wao hawana uwezo wa kuwasomesha.

Amesema kamati hiyo itaongozwa na katibu tawala wa Mkoa na itahusisha wataalamu wa sekta mbalimbali za ujenzi, ununuzi, uhasibu na maofisa wa Takukuru,   kufuatilia mwenendo wa utekelezaji wa miradi inayoanzishwa kwenye halmashauri za Dar es Salaam.

"Watendaji wa halmashauri watatakiwa kutoa ripoti kwenye kamati hiyo kila baada ya wiki mbili, mara mbili kwa mwezi. Hatuwezi kuwa tunacheleweshwa na wanasiasa kwenye halmashauri zetu," amesema Makonda.

Mkuu huyo wa mkoa amesema jana hakupata usingizi baada kumwona Rais Magufuli akizungumzia miradi ya Coco Beach na machinjio ya Vingunguti wakati kila siku anafanya vikao na watendaji wa halmashauri kuhusu miradi hiyo lakini hakuna utekelezaji wowote.

Advertisement

"Jana ilikuwa ni aibu, yaani kwa sababu njaa ni kali kama sio njaa leo ilitakiwa niandike barua ya ku-resign. Sasa nikifikiria njaa iliyopo huko. Naomba sana kila mmoja atimize wajibu wake, ukikwama sehemu waone mamlaka ya juu yako sio unakaa tu," amesema Makonda.

Amesema kamati hiyo itakuwa ikifuatilia miradi kuanzia hatua ya kutangaza tenda mpaka inapokamilika.  Amesema lengo ni kuharakisha utekelezaji wa miradi hiyo ambayo inacheleweshwa na mabaraza ya madiwani kwa maslahi yao binafsi au ya kisiasa.

"Huu mkoa una mafisadi wengi hasa huko kwenye mabaraza ya madiwani. Wengi wa wagombea waliingia wakijua watapiga kama awamu nyingine, wakakuta hali ni ngumu kweli," amesema Makonda.

Advertisement