UCHAGUZI: Makundi kaa la moto Chadema

Mikoani. Uchaguzi wa viongozi ndani ya Chadema hususan ngazi ya majimbo, inaonekana kuwa kaa la moto katika baadhi ya mikoa, lakini mikoa ya Kanda ya Kaskazini ikionekana kukitesa zaidi chama hicho.

Ni kutokana na joto la uchaguzi huo kuwa kali mikoa ya Kaskazini, mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amelazimika kuandika waraka mzito kwenda kwa viongozi wa mikoa hiyo.

Haya yanajiri wakati Msajili wa Vyama vya Siasa akiwa ameipa Chadema siku saba kutoa maelezo ya kwa nini isichukuliwe hatua kwa kutofanya uchaguzi mkuu.

Agizo hilo la msajili linatokana na taarifa kuwa uongozi wa juu wa chama hicho ulimaliza muda wake tangu Septemba 14 hadi sasa hakijafanya uchaguzi, jambo analodai ni kosa kisheria.

Mikoa mingi nchini, Chadema imefanya uchaguzi wa viongozi wa kata kwa kati ya asilimia 70 na 100, lakini majimbo ni kanda chache ambazo zimekamilisha.

Uchunguzi uliofanyika mikoa ya Kilimanjaro, Tanga, Morogoro, Dodoma, Mara, Geita, Mwanza, Manyara na Tanga unaonyesha uchaguzi kwa sehemu kubwa umekamilika ngazi ya kata.

Waraka mzito wa Mbowe

Kutokana na mtifuano mikoa ya Kaskazini, Mbowe amewatumia waraka viongozi wake akisema joto la uchaguzi lililopo lisiporatibiwa kwa weledi kabla ya uchaguzi linaweza kuacha mipasuko.

Mbowe ambaye pia ni kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni (KUB), alibainisha kuwa katika majimbo mengi ya Kaskazini kumekuwepo mnyukano wa makundi.

“Ilihitajika last minute intervention (kuingilia dakika za mwisho) kunusuru umoja wa taasisi yetu,” alisema Mbowe akieleza sababu za kusimamisha uchaguzi Kaskazini.

“Uchaguzi unapokosa usimamizi huru na usiofungamana na upande wowote, hukizika chama mapema. Kama kiongozi mkuu wa Chama, ni wajibu wangu kumlinda kila mmoja wetu, kutoendekeza makundi kwa njia yoyote na kuhakikisha haki inatendeka kwa ukamilifu wake,” amesisitiza Mbowe katika waraka huo.

Kuahirishwa Kaskazini

Mbowe katika waraka huo wenye maneno 611, amesema mikoa ya Kaskazini uliahirishwa pamoja na mambo mengine, kupatanisha makundi yanayohasimiana.

Sababu ya nyingine ni kutoa nafasi ya kufanyika kwa kikao cha mashauriano cha mkoa na kuweka mwafaka wa mtiririko bora na shirikishi kila mkoa.