Malkia wa Nguvu wa darasa la saba 2019

Muktasari:

Pengine leo asingepamba vichwa vya habari kama uongozi wa shule ungekataa ombi la wazazi wake kutaka binti yao afanye mtihani akiwa bado anadaiwa ada ya shule. Na tena si fedha kidogo, ni zaidi ya 500,000.

Dar es Salaam. Pengine leo asingepamba vichwa vya habari kama uongozi wa shule ungekataa ombi la wazazi wake kutaka binti yao afanye mtihani akiwa bado anadaiwa ada ya shule. Na tena si fedha kidogo, ni zaidi ya 500,000.

Ni fedha ambazo wazazi hao wakulima, walilazimika kuzitafuta kwa kudunduliza wakitegemea mauzo ya ndizi wanazolima shambani. Japo hawana kitu, lakini walijua thamani ya elimu, wakabembeleza wakakubaliwa na mtoto akafanya mtihani, hakuwaangusha.

Busara ya uongozi na pengine kwa kujua kuwa binti huyo ni kinara wao wa masomo, ukausukuma uongozi kumruhusu Grace Manga (14) kufanya mtihani wa kumaliza darasa la saba Septemba 11 na 12 mwaka huu.

Mwezi mmoja baadaye Grace akaibeba shule yake ya Graiyaki iliyopo Serengeti mkoani Mara kuwa shule bora kitaifa katika mtihani huo. Lakini pia yeye mwenyewe akaandika historia ya maisha yake kwa kuongoza maelfu ya wanafunzi waliohitimu elimu ya msingi mwaka 2019.

Ukimwona ni mtaratibu, anazungumza kama hataki, kwa kifupi anasema “ndoto yangu ni kuja kuwa daktari kwani ni kazi ninayoipenda.”

Grace au unaweza kumsifu kwa kumuita ‘malikia wa nguvu’ mzaliwa wa Tarime mkoani Mara juzi alitangazwa na Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) kuwa mwanafunzi bora kitaifa katika mtihani wa darasa la saba uliofanyika Septemba 11 na 12.

Mwananchi limezungumza na Grace akiwa shuleni kwake Graiyaki kuhusu safari yake ya elimu hadi alipotangazwa mshindi na kuwaongoza wanafunzi 933,369 waliofanya mtihani huo.

Anasema siri ya mafanikio hayo ni nidhamu, mahudhurio darasani, ushindani darasani, ushirikiano kati ya wazazi na walimu, wanafunzi na jamii. Pia anaitaja sababu nyingine kuwa ni ufanyaji mitihani wa kila wiki shuleni.

Siri nyingine anasema “kuheshimu wazazi wangu na walimu wangu na ushauri wa meneja kwani usipowaheshimu wazazi, walimu au uongozi wa shule huwezi kufanikiwa, kwani wanaweza kuwa wanakwambia fanya hivi wewe hufanyi.”

Grace anasema kitu kingine kilichomfanya kufanya vizuri ni ushindani wa darasani “tulikuwa tunashindana darasani, walikuwa wakinipita na mimi nikiwapita hawajisikii vizuri. Unakazania kuwa katika hiyo namba ili usirudi nyuma.”

Anasema tangu alipoanza darasa la kwanza hakuwahi kushika nafasi nje ya tatu bora.

Akizungumza taratibu na kwa umakini kwa kujibu kila swali, Grace anasema “sikuwa natarajia kama nitakuwa mwanafunzi bora ingawa nilikuwa nasoma kwa bidii na kumuomba Mungu anisaidie niweze kufaulu vizuri mitihani yangu.”

Ilivyokuwa siku ya mitihani

Grace anasema siku ya mtihani, aliamka asubuhi na kujiandaa kisha akaenda katika chumba cha mtihani, ulipofika wakati wa kufanya mitihani akafanya maombi kwa Mungu ili amsaidie.

“Nilivyomaliza kufanya mtihani, nikaufunga mtihani kisha nikamwomba tena Mungu anisaidie,” anasema.

Grace ambaye ni mtoto wa pili kuzaliwa kati ya watatu, anasema alikuwa anatumia muda mwingi kusoma ikiwamo usiku na licha ya wenzake kulala, yeye alikuwa akiamka kujisomea.

Anasema ratiba ya shule walikuwa wanaingia kujisomea saa 11 au 12 jioni hadi saa 4 usiku kisha wanakwenda kulala.

“Hata hivyo mimi ilikuwa nalala hata saa moja au zaidi na ikifika saa saba naamka na wenzangu au mimi mwenyewe. Tukiamka tunajisomea hadi saa tisa kisha tunalala tena hadi saa 10 ambapo tunaamka kujiandaa na kwenda kujisomea tena darasani kwa pamoja kuanzia saa 11 hadi 12 asubuhi,’’ anasema Grace anayekunwa na utendaji wa Rais John Magufuli kwa kuleta maendeleo.

Anasema “ikifika saa 12 asubuhi, mwalimu anaingia kufanya maswali ambayo tumeshindwa hadi saa moja tunakwenda mapumziko na tunarudi saa mbili kuendelea na vipindi vya kawaida.”

Matokeo yalivyotoka

Grace anasema baada ya kumaliza mtihani, alikwenda kwa mama yake mdogo, Neema Selem mkoani Mara akawa anasubiri matokeo ya mtihani huo.

“Sikuwa najua kama matokeo yametoka, mama mdogo (Neema) alipokwenda sokoni, akaja amefurahi akasema umefaulu.”

“Aliponiambia nilifurahi sana na nikamshukuru Mungu, nikasema ndoto zangu zimetimia,” anasema Grace.

Anasema baada ya kupata taarifa hizo, alimpigia simu mama yake anayeitwa Mary kumjulisha kuhusu matokeo hayo, “mama akaniambia asante, uongeze bidii na akaniahidi kuninunulia zawadi.”

Mama azungumza

Mary Imori, mama mzazi wa Grace anasema “nilifurahi sana binti yangu kufaulu, sikutegemea kwa kweli ila nilijua tu mwanangu ana uwezo na anafanya vizuri darasani.”

Ni zawadi gani ambayo amemuahidi mwanae? Mary anasema “mimi napenda kumwahidi na akiniambia nimnunulie namnunulia na mara nyingi nilikuwa namnunulia vitabu kwani anapenda sana kusoma, hata kitandani kwake utakuta kuna vitabu.”

Mary anatoa nasaha kwa wazazi wenzake kujenga utamaduni wa kuwapatia zawadi watoto wao. “Wakazanie watoto si kuwapa mambo ambayo hayawajengei msingi, wawe na maadili na wawape vitabu kwani humjenga mtoto katika makuzi mazuri,”anasema.

Kuhusu gharama za kumsomesha mtoto wake anasema yeye na mume wake ni wakulima na wamekuwa wakipata kipato kutokana na mazao wanayolima kama migomba ya ndizi na mahindi.

“Gharama ya kumsomesha tunajitahidi sana, tuna shamba la migomba, zinapokuwa zimeiva natunza kidogo kidogo, nikivuna mahindi natunza na nikikwama kidogo nakwenda kumwomba meneja (wa shule) naye anatusikiliza,” anasema Mary

“Hata mtihani wa taifa ulipofika, tulikuwa bado tunadaiwa Sh550,000 tukamwomba meneja akakubali, akafanya mtihani na sherehe yao, tukalipa kisha tukamchukua. Kwa hiyo tumekuwa tukijibana ili kutimiza ndoto zake, anasema Mary.