Mamia waandamana Dar kushinikiza ndege ya Tanzania iliyozuiwa Afrika Kusini kuachiwa

Moja ya mabango walilokuwa wamebeba watu waliokusanyika  leo katika Ubalozi wa Afrika kusini nchini kwa ajili ya kushinikiza ndege iliyokamatwa iachiwe

Muktasari:

Takribani watu 100 leo Jumatano Agosti 28, 2019 wameandamana kwenda  ubalozi wa Afrika Kusini nchini Tanzania kushinikiza ndege ya Air Tanzania iliyozuiwa nchini humo kuachiwa.

 


Dar es Salaam. Takribani watu 100 leo Jumatano Agosti 28, 2019 wameandamana kwenda  ubalozi wa Afrika Kusini nchini Tanzania kushinikiza ndege ya Air Tanzania iliyozuiwa nchini humo kuachiwa.

Ndege hiyo iliyokuwa inatoka Afrika Kusini kwenda jijini Dar es Salaam, Tanzania Agosti 23, 2019 ilizuiwa kuruka kwa amri ya Mahakama Kuu ya Gauteng, Johannesburg nchini Afrika Kusini.

Huku wakiwa na mabango yenye ujumbe mbalimbali kuhusu  Tanzania ilivyoisaidia Afrika Kusini kudai uhuru wake, watu hao wamesema kuzuiwa kwa ndege hiyo si jambo sahihi.

“Tunataka ndege yetu, tunataka ndege yetu,” ndivyo walivyosikika wakiimba watu hao huku wakieleza zilipo ofisi za ubalozi huo eneo la Posta katikati ya Jiji la Dar es Salaam.

Wakati wakiwa wanatembea huku wamebeba mabango, askari polisi nao walikuwa na bango la tahadhari, wakiwataka kutawanyika.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa akizungumza baada ya kuwatawanya waandamanaji hao amesema, “Tumewakamata wale ambao wameratibu na kuongoza maandamano hayo, Chochote ambacho wanataka kupeleka kwa umma, wanaweza kuandika barua au kutuma wawakilishi.”

Amesema Serikali ya Tanzania imepeleka watu Afrika Kusini kushughulikia suala hilo, kuwataka Watanzania kuwa watulivu, wasubiri hatua zitakazochukuliwa.

“Hili ambalo wamelifanya la kuandamana halikubaliki. Tuheshimu sheria hata pale tunapoona jambo linafanyika halipendezi lakini kuheshimu sheria ni jambo la maana sana,” amesema Mambosasa.

Juzi msemaji wa Serikali ya Tanzania, Dk Hassan Abbas amesema ndege hiyo imezuiwa  kutokana na kesi ya madai iliyofunguliwa na Hermanus Steyn.

Steyn,  raia wa Afrika Kusini anadai fidia baada ya mali zake kutaifishwa na Serikali ya Tanzania mwaka 1980.

Ndege hiyo aina ya Airbus A220-300 imeshikiliwa katika uwanja wa Oliver Tambo jijini Johannesburg baada ya kufanya safari kadhaa tangu Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) lianze kufufua ruti zake za nje ya nchi.

Katika maelezo yake Dk Abbas amesema Steyn aliridhia mali hizo kutaifishwa lakini hoja ikaja alipwe fidia kiasi gani.

“Ndege zetu zipo salama kwa maana ya ndege sita ambazo Air Tanzania kwa sasa inaziendesha isipokuwa hii moja ambayo tumetoa taarifa kuwa imezuiwa kwa ajili ya kesi.”

“Watu wanahusisha jambo hili na madeni ya zamani kwenye shirika  kati ya Air Tanzania na Shirika la ndege Afrika ya Kusini. Niseme tu kuwa hii kesi haihusiani kabisa na hilo,” amesema Dk Abbas.

Ameongeza, “Alikuwa (Steyn) na mashamba, mifugo na mali nyingi kwa hiyo Serikali kwa wakati huo ikaona ni sahihi hizi mali zitaifishwe kwa hiyo ukitaka kuchimbua mgogoro huu asili yake unatoka miaka ya 1980.”

Amesema ilipofika miaka ya 1990 walikubaliana fidia atakayolipwa, miaka ya 2000 akalipwa na kuna kiasi kilichobaki ambacho mhusika amefungua kesi akitaka amaliziwe kulipwa.

“Ukiangalia awamu zote (za uongozi) kulikuwa na makubaliano, ukiangalia hatua za kimahakama wanakubaliana lakini malipo hayakufanywa lakini yalikuja kufanyika katika awamu ya nne,” amesema Dk Abbas.

Dk Abbas amesema mdai  huyo amekwenda Afrika Kusini kwa taratibu za mahakama, akibainisha kuwa zipo nchi ambazo mtu anaruhusiwa kuiomba hukumu ya nchi nyingine itekelezwe kwenye nchi aliyopo, akisisitiza kuwa ni  taratibu za kawaida kwenye sheria.

“Sisi tunaheshimu utawala wa sheria kwa sababu ni mfumo wa kawaida. Sheria itafuata mkondo wake, ukisoma ile hukumu inaturuhusu kuipinga.”

“Nafikiri  wanasheria wetu wataichambua na wataona hatua gani za kuchukua lakini ni mfumo wa kisheria ambao Serikali tunaufuata na tunauheshimu. Tunawahakikishia Watanzania kuwa tunasimamia maslahi ya Taifa,  ndege yetu itarudi na itaendelea na shughuli zake za kawaida,” amesema Dk Abbas.

Amesema kesi ya msingi haijasikilizwa kwa sababu anayedai fidia  ametumia sheria za Afrika Kusini kuomba kutekeleza hukumu ya nchi nyingine.

“Kesi ya msingi ya kiasi kilichobaki kwamba tukilipe haikusikilizwa, yeye aliomba maombi madogo ambayo pia yana sehemu mbili,  kusikilizwa wote (Serikali ya Tanzania na mdai) na mahakama au kusikilizwa yeye mwenyewe kama alivyofanya,” amesema Dk Abbas.

Kushikiliwa kwa ndege hiyo kunarejesha kumbukumbu ya ndege nyingine ya Tanzania aina ya Bombardier Q400-8 iliyozuiwa nchini Canada mwaka 2017 kutokana na madai ya Sh87.3 bilioni zilizokuwa zikidaiwa na kampuni ya kikandarasi.