VIDEO: Mamia wajitokeza kushiriki Jukwaa la Fikra la Mwananchi

Washiriki wa Jukwaa la Fikra wakiwa wamejaa kwenye Ukumbi wa Kissenga tayari kwa kujadili namna ya kuwawezesha vijana kuwa na ujuzi na maarifa mahsusi, jijini Dar es Salaam leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

  • Zaidi ya watu 600 wameshiriki  mjadala wa vijana na elimu katika jukwaa maalum maarufu kama Mwananchi Jukwaa la Fikra linalofanyika katika ukumbi wa Kisenga jijini Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Zaidi ya watu 600 wameshiriki  mjadala wa vijana na elimu katika jukwaa maalum maarufu kama Mwananchi Jukwaa la Fikra linalofanyika katika ukumbi wa Kisenga jijini Dar es Salaam.

Mjadala huo unaorushwa moja kwa moja na MCL Digital na televisheni ya ITV umeanza saa 3: 00 usiku leo Alhamisi Septemba 19, 2019.

Idadi hiyo ya watu ambao baadhi wamelazimika kufuatilia wakiwa nje ya ukumbi, imezungumziwa na mkurugenzi mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communication Ltd (MCL), Francis Nanai akibainisha  kuwa mada imewavutia wengi na ina umuhimu kwa Taifa.

Mada katika Jukwaa hilo ni kuwawezesha vijana kuwa na ujuzi  kwa kuzingatia mada ndogo za ukuzaji wa mtalaa, mfumo wa uwasilishaji wa mtalaa, ufadhili wa elimu pamoja na uhusiano baina ya taasisi za elimu dhidi ya soko la ajira.

Akizungumza katika ufunguzi, Nanai amesema katika mada ya leo zaidi ya watu 600 wameshiriki.

“Hii ni mara ya tano tunafanya mkutano kama huu lakini leo niseme ‘nyomi’ imeitikia kwelikweli, hii ‘nyomi’ ni kubwa, maana ukumbi huu unachukua watu 500 lakini leo nimeona viti vinaongezwa.”

“Na wengine wako nje wamekosa nafasi ya kuingia ndani imebidi wawekewe ‘screen’ ili wafuatilie tukio kinaloendelea huku ndani. Hii ni furaha kwetu na ni ishara kuwa mada hii inavutia, ni mada ambayo ina umuhimu katika taifa letu,” amesema Nanai.

Amewaomba watakaopata fursa ya kuchangia mada kutumia muda vizuri ili kutoa nafasi kwa wenzao.