LIVE: Mamia wamuaga Mufuruki Dar

Muktasari:

Mamia ya waombolezaji wamejitokeza katika ukumbi wa kimataifa wa Julius  Nyerere (JNICC) leo Jumanne Desemba 10, 2019 kuaga mwili wa mfanyabiashara maarufu nchini Tanzania, Ali Mufuruki.


Dar es Salaam. Mamia ya waombolezaji wamejitokeza katika ukumbi wa kimataifa wa Julius  Nyerere (JNICC) leo Jumanne Desemba 10, 2019 kuaga mwili wa mfanyabiashara maarufu nchini Tanzania, Ali Mufuruki.

Mwili wa Mufuruki aliyefariki dunia juzi alfajiri uliwasili nchini jana jioni ukitokea Afrika Kusini, baada ya kuagwa leo  utazikwa katika makaburi ya Kisutu, jijini Dar es Salaam.

Viongozi, wastaafu, wafanyabiashara na wananchi wamejitokeza katika ukumbi huo idadi ambayo inaibua tafsiri kuwa mfanyabiashara huyo alikuwa akigusa maisha ya wengi.

Miongoni mwa waombolezaji ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji), Angela Kairuki; Waziri Mkuu mstaafu, Joseph Warioba na aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Charles Mwijage.

Wengine ni Katibu Mkuu mstaafu wa CCM, Abdulrahman Kinana; Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Joseph Sokoine; mbunge wa Muleba Kusini (CCM), Profesa Anna Tibaijuka na mkurugenzi wa taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku.

Pia wapo mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya Mwananchi Communication Limited (MCL),  Francis Nanai na  mkurugenzi wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF),  Godfrey Simbeye.

Mufuruki aliyezaliwa Novemba 15, 1958 amekuwa mwenyekiti na mjumbe wa zaidi ya bodi 30 za kampuni mbalimbali katika kipindi cha miaka 25.

Mufuruki alifunga ndoa na Saada Ibrahim Aprili 16, 1993 na kujaaliwa kupata watoto wanne ambao ni Laila, Zahra, Sophia na Tegegne.

Katika ukumbi huo ulinzi umeimarishwa na kabla ya kuingia kuna  eneo maalumu limetengwa na kuwekwa  kitabu cha kusaini kilichowekwa na picha ya mfanyabiashara huyo.

Ndani ya ukumbi kuna bango kubwa lililowekwa picha zake mbili na meza ambayo litawekwa jeneza lake.