Maombi ya Bob Wangwe kwa jaji mkuu wa Tanzania

Mwanaharakati wa haki za binadamu nchini Tanzania, Bob Wangwe

Muktasari:

  • Mwanaharakati wa haki za binadamu nchini Tanzania, Bob Wangwe amewasilisha maombi matatu kwa Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma.

Dar es salaam. Mwanaharakati wa haki za binadamu nchini Tanzania, Bob Wangwe amewasilisha maombi matatu kwa Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma.

Ombi la kwanza ni kutaka kurejeshewa faini ya Sh5 milioni aliyotoa baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kumkuta na hatia katika mashtaka ya uchochezi. Wangwe alikata rufaa Mahakama Kuu kupinga hukumu hiyo na kushinda.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi Januari 23, 2020 jijini Dar es Salaam, Wangwe amesema licha ya kufuata taratibu zote hadi sasa pesa hiyo hajarejeshewa.

"Ombi la pili ni ucheleweshaji wa majibu ya mwanasheria mkuu wa Serikali katika kesi ya kikatiba niliyofungua mwaka 2018 katika mahakama kuu ya Arusha," amesema Wangwe.

Amefafanua kuwa msingi wa kesi hiyo unalenga kuomba msimamo wa mahakama endapo kifungu cha 16 cha sheria ya makosa ya mtandao hakipingani na ibara ya 18 ya katiba ya Tanzania.

Kutokana na mazingira hayo, Wangwe amesema jambo la tatu ni kumshauri Jaji mkuu kufanya mapitio ya mfumo wa utoaji haki nchini kwa kuunda tume itakayomsaidia kupunguza udhaifu uliopo katika muhimili huo.