Marekani yampongeza Magufuli, yasisitiza tume huru ya uchaguzi

Muktasari:

Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania leo Ijumaa Januari 31, 2020 umempongeza  Rais John Magufuli baada ya kiongozi mkuu huyo wa nchi kueleza kuwa uchaguzi mkuu wa Oktoba, 2020 utakuwa huru na haki.

Dar es Salaam. Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania leo Ijumaa Januari 31, 2020 umempongeza  Rais John Magufuli baada ya kiongozi mkuu huyo wa nchi kueleza kuwa uchaguzi mkuu wa Oktoba, 2020 utakuwa huru na haki.

Mbali na pongeza hizo, ubalozi huo umetaka kuharakishwa kwa  uanzishwaji wa tume huru ya uchaguzi.

Januari 21, 2020 Rais Magufuli aliwahakikishia mabalozi wanaoziwakilisha nchi zao Tanzania kuwa uchaguzi huo utakuwa huru na wa haki, alipokuwa akizungumza nao Ikulu Dar es Salaam.

Kauli hiyo ya Magufuli iliibua mjadala miongoni mwa vyama vya siasa na wanaharakati wa demokrasia wakihoji uwezekano huo bila kuwepo kwa tume huru ya uchaguzi.

Katika taarifa ya ubalozi huo iliyotolewa leo Ijumaa Januari 31, 2020 ubalozi huo umeonyesha kutiwa moyo na kauli ya kiongozi mkuu huyo wa nchi.

 “Tunatoa wito wa kuharakishwa kwa zoezi la uandikishaji wapiga kura lenye uwazi, kuanzishwa kwa tume huru ya uchaguzi na kuteuliwa mapema kwa waangalizi wa uchaguzi wa kitaifa na wa kimataifa wa kuaminika watakaofuatilia uchaguzi kwa kipindi kirefu na kipindi kifupi,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.

Ubalozi huo pia umesema unatarajia kuwepo kwa uchaguzi wa amani ambao wagombea wote watakutana kwa amani wakieleza mawazo yao na kampeni zitakazofanyika katika misingi ya usawa.