Margaret Sitta kupokea joho la marehemu mumewe

Muktasari:

Joho la Spika wa Bunge la tisa marehemu Samuel Sitta litapokewa kesho Jumanne Januari 28, 2020 na mkewe Margaret Sitta ambaye ni mbunge wa Urambo (CCM).

Dodoma. Joho la Spika wa Bunge la tisa marehemu Samuel Sitta litapokewa kesho Jumanne Januari 28, 2020 na mkewe Margaret Sitta ambaye ni mbunge wa Urambo (CCM).

Margaret ataungana na maspika wastaafu,  Pius Msekwa na Anne Makinda kupokea majoho waliyoyatumia wakati wakiongoza chombo hicho cha Dola kwa nyakati tofauti.

Taarifa iliyotolewa leo Jumatatu Januari 27, 2020 na Spika Job Ndugai inaeleza kuwa Bunge limeamua kuwapa heshima maspika wastaafu kwa kuwakabidhi majoho waliyokuwa wakiyatumia.

Marehemu Sitta anakumbukwa kutokana na uhodari wa kuongoza Bunge na katika kipindi chake Edward Lowassa alijiuzulu uwaziri mkuu.

Shughuli hiyo ya kukabidhi majoho itafanyika kesho katika kikao cha kwanza cha mkutano wa 18 wa Bunge.

"Joho alilolitumia Samuel Sita litapokelewa na mkewe kwa niaba ya familia ya marehemu Sitta na wengine watapokea wenyewe,” amesema Ndugai.