VIDEO: Mashinji akwamisha kesi ya vigogo Chadema

Muktasari:

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam imeshindwa kuendelea kusikiliza  kesi ya uchochezi inayowakabili viongozi tisa wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania cha Chadema akiwemo Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe baada ya mmoja wa washtakiwa katika kesi hiyo kutokuwepo.

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam nchini Tanzania imeshindwa kuendelea kusikiliza kesi ya uchochezi inayowakabili viongozi tisa wa chama kikuu cha upinzani nchini humo cha Chadema akiwemo Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe.

Hatua hiyo inatokana na mmoja wa washtakiwa katika kesi hiyo, Dk Vicent Mashinji ambaye ni Katibu Mkuu wa Chadema kushindwa kufika mahakamani hapo kusikiliza kesi yake.

Dk Mashinji ameshindwa kufika mahakamani hapo kwa sababu anahudhuria kesi yake nyingine iliyopo Mahakama ya Hakimu Mkazi Songea mkoani Ruvuma.

Wakili wa utetezi, Profesa Abdallah Safari ameieleza mahakama hiyo leo, Jumanne Septemba 24, 2019 wakati kesi hiyo ilipoletwa kwa ajili ya washtakiwa kuanza kujitetea baada ya kukutwa na kesi ya kujibu.

Profesa Safari amedai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Thomas Simba kuwa, Dk Mashinji ameletewa wito wa kuitwa mahakamani kuhudhuria kesi yake ya  jinai namba 9/2017 iliyopo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Songea.

"Kwa mujibu wa barua hii ya wito, Dk Mashinji alitakiwa kuripoti mahakamani hapo na kuhudhuria kesi yake, Septemba 23, 2019, hivyo kwa sababu hiyo tunaomba  kuahirisha kesi hiyo Oktoba 7 na 8, 2019 " amedai Profesa Safari.

Katika hatua nyingine, Profesa Safari amewasilisha maombi mawili, akiomba  wateja wake wawili ambao ni Ester Matiko na Dk Mashinji kuhudhuria mikutano nje ya nchi.

Katika ombi la kwanza, Matiko anatakiwa kuhudhuria mkutano huko Kigali nchini Rwanda unaoanza Septemba 25 hadi 28, 2019.

"Matiko pia ana mwaliko mwingine wa mkutano kutoka Brussels nchini Belgium, ambao unatarajia kuanza Oktoba 13 hadi 18, 2019," alidai Profesa Safari

"Kupande wake, Dk Mashinji yeye anatakiwa kwenda nchini Uingereza kuhudhuria mkutano unaotarajia kufanyika Septemba 26 hadi Oktoba 6, 2019, hivyo tunaomba kesi hii iahirishwe hadi Oktoba 7 na 8, mwaka huu," amedai Profesa Safari bila kufafanua mikutano hiyo inahusu nini.

Awali, wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi ameieleza mahakama kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya washtakiwa kuanza kujitetea.

"Washtakiwa wote wapo ndani ya mahakama isipokuwa mshtakiwa Dk Vicent Mashinji, haonekani mahakamani, hivyo tunaomba upande wa utetezi watueleze alipo" amedai Nchimbi

Hata hivyo, Wakili Nchimbi amepinga maombi ya ruhusu yalitolewa na upande wa utetezi kwa maelezo yana upungufu.

Hakimu Simba baada ya kusikiliza hoja za pande zote, ameahirisha kesi hiyo hadi kesho Jumatano atakapotoa uamuzi.

Tayari mashahidi wanane wa upande wa mashtaka wameshatoa ushahidi wao dhidi ya washtakiwa hao.

Mbali na Mbowe, washtakiwa wengine katika kesi hiyo  ni wabunge;

Esther Matiko (Tarime MJini), Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini), John Heche (Tarime Vijijini), Halima Mdee (Kawe), Ester Bulaya (Bunda Mjini), John Mnyika wa Kibamba pamoja na Naibu Katibu Mkuu- Zanzibar, Salum Mwalimu.

Washtakiwa kwa pamoja  wanakabiliwa na mashtaka 13 yakiwemo ya uchochezi.