Matarajio ya wananchi katika Bajeti

Thursday June 13 2019

 

By Waandishi Wetu, Mwananchi [email protected]

Dar/mikoani. Wakati Serikali ikiwasilisha bajeti yake ya mwaka wa fedha wa 2019/20 inayofikia Sh33 trilioni leo jioni, baadhi ya Watanzania wameelezea matarajio yao katika bajeti hiyo ya tatu katika utawala wa Rais John Magufuli.

Baadhi ya mambo ambayo wananchi hao wameyagusia walipohojiwa na waandishi wetu kwa nyakati tofauti jana ni pamoja kuonyesha mwelekeo wa kupunguza ugumu wa maisha wakitaraji pia kwamba itaonyesha ushiriki wa Serikali katika kusisimua sekta binafsi na kuendelea kuchochea uchumi wa viwanda.

Pamoja na hayo, baadhi yao walisema wameshindwa kufuatilia kwa kina Bunge la Bajeti kutokana na kutoonyeshwa moja kwa moja wakisema hiyo imewafanya kutojua kinachoendelea.

Mfanyabiashara ndogondogo katika Mtaa wa Nyerere jijini Mwanza, Medard Alex alisema masuala ya bajeti yanahitaji wananchi kushirikishwa kuanzia uandaaji, mipango ya vipaumbele na utekelezaji wa bajeti na wananchi kufuatilia.

“Serikali kuzuia bunge live (vikao vya bunge kuonyeshwa moja kwa moja) kumesababisha tushindwe kujua na kufuatilia wanachojadili wawakilishi wetu ikiwamo bajeti,” aliongeza Robert George mkazi wa Nyegezi.

Akizungumzia matarajio ya bajeti ijayo, Emiliana Bujingwa wa Mwanza alisema inatakiwa kushughulikia suala la mfumuko wa bei aliyosema inaongeza ugumu wa maisha kwa wananchi wa kawaida.

Advertisement

Mkoani Shinyanga, Self Rashid kutoka Wilaya ya Kishapu alisema matarajio yake katika bajeti ijayo ni kuona mwananchi wa kipato cha chini anamudu gharama za maisha hasa wale wa maeneo ya vijijini.

Rehema Fanuel, wa Manispaa ya Shinyanga alisema bajeti nyingi kila mwaka huwa na mambo yaleyale, hivyo Serikali itakavyokuwa imepanga wao wako tayari kupokea.

Mkoani Geita wananchi waliohojiwa walionyesha matumaini. Boaz Mazigo alisema anatarajia kuongezeka kwa uboreshwaji wa miundombinu ikiwemo ya afya, barabara na elimu.

Jijini Dodoma, wananchi waliohojiwa walisema wanatarajia bajeti hiyo itaangalia uhalisia wa maisha ya Watanzania wa kawaida na kutoa njia za kumudu gharama za maisha.

Mkazi wa Dodoma, Faustine Mwakalinga alisema matarajio yake ni kuona bajeti hiyo inamwangalia Mtanzania wa chini ili nayeye aweze kumudu maisha yake ya kila siku.

“Hata katika suala la kukusanya mapato, wawe wanawakadiria wafanyabiashara kodi inayolingana na mitaji yao na sio kuwawekea kadirio kubwa ambalo linaenda kuua mitaji yao,” alisema Mwakalinga.

Jijini Arusha, wakazi, wafanyabiashara, wawekezaji na wananchi wa kawaida waliohojiwa walisema wana matumaini makubwa na bajeti hiyo wakiamini kwamba itazingatia maoni ya sekta binafsi katika kuondoa vikwazo vya kibiashara na ili nayo ishiriki vyema katika kukuza uchumi

Katibu Mtendaji wa Chama cha Mawakala wa Utalii Tanzania (Tato), Sirili Akko alisema wana imani kubwa kwamba maoni yao katika kukuza sekta binafsi yatakuwepo katika bajeti.

“Sisi kazi ya kutoa maoni yetu tumemaliza na tuna mategemeo katika bajeti kusikia jinsi ambavyo Serikali imejipanga kuimarisha uhusiano na sekta binafsi katika dhana nzima ya kukuza uchumi na kuondoa kero” alisema.

Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara, Wenye Viwanda na Kilimo (TCCIA), Mkoa wa Arusha, Walter Maeda pia alisema, kwamba wameshatoa maoni na sasa wanasubiri bajeti kwa hamu kubwa.

Mfanyabishara katika Barabara ya Kitope, Anna Makulu alisema kama bajeti hiyo itashusha bei ya umeme na petroli, itasaidia kwani bidhaa wanazouza watazisafirisha kwa gharama nafuu.

Mkoani Kilimanjaro baadhi wananchi wameitaka Serikali kufanya kazi na sekta binafsi.

“Serikali ikitumia fedha za kutosha na kufanya kazi na sekta binafsi, fedha zitaonekana mitaani, kwani mpaka sasa tunavyoongea mzabuni mkubwa katika uchumi wetu ni Serikali,” alisema Priscus Tarimo, mkazi wa Moshji mjini.

Mfanyabiashara wa Moshi mjini John Benedict ameiomba Serikali kuondoa kodi ya kuagiza mitambo nje ya nchi.

Mkazi wa Mtaa wa Mzimuni, Segerea, Abdulfatah Lyeme alisema anatamani kuona fungu la bajeti ya miradi ya maendeleo linakwenda kulipa madeni ya makandarasi wa ndani.

Mwalimu Lilian Sawia alisema ili kuimarisha mazingira ya upatikanaji wa elimu bora kwa Watanzania, Serikali kupitia inatakiwa kuwekeza kwenye upatikanaji wa walimu.

Mkazi wa Kibaha Neema Komu alisema, “hali ya upatikanaji wa pesa hivi sasa ni ngumu hivyo matarajio yangu ni kuwa Serikali itashusha bei ya bidhaa muhimu kama sukari na mafuta ili kurahisisha maisha ya wananchi.”

Mjasiriamali wa wilayani, Mafinga, Iringa, Khamisi Thobias alisema: “natamani bajeti hiyo iangalie huduma za afya.”

Imeandikwa na Ngollo John, Johari Shani na Stella Ibengwe Rachel Chibwete,Mussa Juma, Florah Temba na Janeth Joseph,Mwananchi, Sanjito Msafiri, Kelvin Matandiko na Fidelis Butahe.

Advertisement