Mawakala wa Chadema Serengeti waapishe sehemu moja

Mawakala wa Chadema jimbo la Serengeti wakijaza fomu za kiapo. Picha na Anthony Mayunga

Muktasari:

Chadema yasema wameamua kuwaapisha mawakala sehemu moja ili kama kuna tatizo walitatue kwa pamoja

Serengeti.  Licha ya msimamizi wa Jimbo la Serengeti kuweka vituo  katika kata mbalimbali ili kuwapunguzia gharama na usumbufu kwa mawakala Chama cha Demokrasia na Maendeleo  (Chadema), wao wameamua kiapo cha mawakala wao kufanyikia sehemu moja wilayani.

Jimbo hilo lina kata 30 na vituo vya kupigia kura 408.

Msimamizi wa uchaguzi jimbo hilo, Juma Hamsini leo Jumatano Oktoba 21 akiwaapisha mawakala amesema wameleta mawakala 500 wakiwamo wa vituo 408,wa ziada na wale wa majumuisho kwa ajili ya kuapishwa eneo moja tofauti na vyama vingine ambavyo wanaapa kwenye maeneo waliko.

"Sisi hatuna pingamizi na uamuzi wao ndiyo maana tumeamua kuwaapisha pamoja, lengo la kuweka maeneo tofauti tuliangalia gharama za kuwasafirisha na kuwalisha na vyama vingi vimedai havina uwezo, tunawashukuru kwa kuwa tumefanya kwa wakati mmoja na kumaliza, "amesema.

Katibu wa  Chadema, Julius Antony amesema wao wameamua kufanyia sehemu moja ili kama kuna tatizo walitatue kwa pamoja maana viongozi hawataweza kukigawa kuzunguka kila kata au tarafa.

Kazi hiyo imefanywa na kila chama kwa wakati wake na mawakala walioapishwa ni CCM, Chadema, ACT Wazalendo, CUF na NCCR Mageuzi.