Mawaziri kuanza kujibu hoja za Mpango wa Maendeleo 2020/2021

Muktasari:

  • Mapendekezo ya Mpango huo yaliwasilishwa bungeni na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango Jumanne wiki iliyopita na kujadiliwa kwa siku tano. Miongoni mwa hoja zilizotikisha katika mjadala huo ni pamoja na ile ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa, mawaziri na watalaamu washtakiwe kwa uhujumu uchumi wakishindwa kusimamia fedha za miradi.

Dodoma. Bunge kesho Jumatatu Novemba 11, 2019 litaendelea na vikao vyake huku mawaziri wakitarajiwa kujibu hoja zilizotolewa na wabunge wakati wakichangia Mpango wa Maendeleo wa Taifa na Mwongozo na Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya 2020/2021.

Mapendekezo ya Mpango huo yaliwasilishwa bungeni na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango Jumanne wiki iliyopita na kujadiliwa kwa siku tano.

Miongoni mwa hoja zilizotikisha katika mjadala huo ni pamoja na ile ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa, mawaziri na watalaamu washtakiwe kwa uhujumu uchumi wakishindwa kusimamia fedha za miradi.

Nyingine ni bajeti ya kilimo kutopelekwa kama ilivyopitishwa na Bunge, kutotekelezwa kwa mipango iliyopita na urasimu katika biashara.

Hoja ya uchaguzi wa Serikali za mitaa ilijadiliwa na wabunge wengi katika siku hizo tano kuliko hoja nyingine zilizoko katika mpango huo.

Miongoni mwa wabunge walioibua hoja hiyo ni Peter Msigwa (Iringa Mjini-Chadema), John Heche (Tarime Mjini- Chadema), Deo Sanga (Mufindi Kaskazini-CCM), Seleimani Bungara (Kilwa Kusini-CUF) na Ritta Kabati (Viti Maalum–CCM).

Bungara alisema nchi imefika pabaya kwa mikutano ya vyama kuzuiliwa, matukio ya kutekwa watu na mauaji.

“Leo katika Wilaya yake ya Kilwa amesimamisha wagombea katika uchaguzi wa Serikali za mitaa 15 lakini wameondolewa wote. Katika kijiji kimoja cha Nachilinji waliondolewa kwasababu hawajui kusoma kingereza,”alisema.

Kabati alisema haoni ajabu kwa wagombea wa upinzani kujitoa katika uchaguzi huo kwasababu miradi mingi iliyotekelezwa na CCM imeonyesha jinsi kilivyo makini katika kuongoza.

Katika hoja nyingi Mbunge wa Manyovu (CCM) Arbert Obama alitaka mawaziri na watalaam watakaoshindwa kusimamia fedha za miradi ya maendeleo washtakiwe kwa makosa ya uhujumu uchumi.

“Wizara ilikuwa wapi?Wataalamu walikuwa wapi? Mkuu wa wilaya alikuwa wapi? Mkuu wa Mkoa alikuwa wapi? Waziri wa kisekta alikuwa wapi? Miradi mingi tunayopeleka fedha inakuwa haina tija,”alisema Obama.

Mbunge wa Viti Maalum (Chadema) Sophia Mwakagenda alisema mwaka 2019/2020 walipanga Sh 100bilioni ziende katika kilimo lakini fedha iliyotoka ni Sh 2bilioni tu.

“Ili uweze kufanikiwa katika viwanda unatakiwa kuwekeza katika kilimo ambacho ndicho kinatoa malighafi. Usipofanya hivyo unakuwa bado unafanya siasa katika mambo makini,” alisema.

Hoja ya kutotekelezwa kwa mpango wa maendeleo wa Taifa, imezungumzwa na James Mbatia (NCCR- Mageuzi) na David Silinde (Momba-Chadema) ambaye alisema kuna miradi ya vielelezo ambayo iko katika Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa miaka mitano lakini imeshindwa kutekelezwa.

Alitaja miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa bandari mpya ya Bagamoyo, uanzishaji wa kituo cha biashara kurasini, uanzishwaji wa kiwanda cha kuunda magari na kutengeneza vipuri, miradi ya Mchuchuma na Liganga.

Kuhusu urasimu katika biashara,wabunge CCM Ritta Kabati (Viti-Maalum) na Charles Kitwanga(Misungwi) ambaye aliitaka watendaji kupunguza urasimu katika biashara ili kuwawezesha watu wengine kuwekeza nchini.

“Hebu tupunguze huu urasimu…anayejenga kiwanda hapa nchini hatakinyanyua na kuondoka nacho. Na kama anaondoka tuwape wataalam kiwanda wakiendeshe,” alisema Kitwanga.

Wiki hii mbali na maswali na majibu, wabunge watajadili maazimio saba na Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali namba 7 wa Mwaka 2019.

Muswada huo pamoja na mambo mengine unapendekeza kufanyiwa kwa marekebisho kwa Sheria ya Usimamizi na Udhibiti wa VVU na Ukimwi.

Katika marekebisho hayo Serikali inapendekeza kuweka umri wa mtoto kupima Virusi vya Ukimwi (VVU).