Mbagala wajitokeza kuchangia damu MOI, uniti 1000 zapatikana

Saturday January 11 2020

 

By Peter Edson, Mwananchi, [email protected]

Dar es Saalam. Taasisi ya Mifupa (MOI), imekusanya  zaidi ya Uniti 1000 za damu  katika kambi  iliyofanyika leo january 11, 2020, Jijini  Dar es Salaam, lengo likiwa ni kunusuru maisha ya wagonjwa wanaofariki kwa kukosa damu.

Damu hiyo imekusanywa   baada  wanachama wa  Taasisi ya Familia   ya amani Duniani FFWPU kujitokeza kuchangia  ikiwa ni siku chache baada ya taasisi ya MOI kutangaza kuwa benki ya damu hospitalini hapo imepungua 

Akizungumza January 11, 2020 jijini Dar es Salaam Msemaji wa MOI Patrick Mvungi  amesema taasisi hiyo inauhitaji mkubwa  wa damu kwa ajili ya watu kufanyiwa upasuaji

“Tulishirikiana na Shirika hili kutoa hamasa kwa wananchi na watu wengi wamejitokeza kwa kiwango kikubwa na idadi hii haijawahi kutokea tangu kuanzishwa kwa taasisi hii”amesema Mvungi.

Mvungi amesema  katika utoaji wa huduma wamejipanga kuhakikisha kuwa wanatoa huduma kwa weledi lakini changamoto kubwa inayowakabili ni upatikanaji wa damu.

“Hakuna  mgonjwa aliyewahi kupoteza maisha kutokana na ukosefu wa damu, tunautaratibu wa kuwahudumia wagonjwa na tunahakikisha  kunaupatikanaji wa damu katika taasisi na matumizi yetu kwa siku ni chupa 16”amesema Mvungi.

Advertisement

Kwa  Upande wake Kiongozi Mkuu wa kitaifa wa FFWPU  Stylos Simba amesema wameshiriki matendo hayo ya huruma baada ya waliamua kuhamasisha wananchama wake kujitolea damu kutokana na changamoto ya damu iliyotangazwa katika taasisi hiyo.

“Baada ya kuonana na uongozo wa MOI niliwaahidi kuwa wanachama wetu zaidi ya 1000 kutoka Mbagala watakuja kuchangia damu, si kwa sababu wanapenda bali ni kunusuru Maisha ya watanzania, “alisema.

Amesema hamasa hiyo ya wananchi imetokana na elimu waliyoitoa kwa wananchi  juu ya umuhimu wa kuchangia damu ili kuokoa Maisha ya wengine.

“Leo wanachama wetu kutoka mbagala wamekuja lakini tunawanachama wengi kutoka maeneo mengine watakuja hapa kuchangia damu ili kuunga mkono juhudi za serikali katika uimarishaji wa huduma za afya na pia wanachama wetu wengine wataenda kutoa huduma zingine za afya mkoani Morogoro”amesema Simba

 

Advertisement