Mbaroni kwa mauaji ya mama na mtoto, waliahidiwa Sh2.2 milioni

Kamanda wa Polisi mkoa wa Shinyanga, Richard Abwao

Muktasari:

Polisi mkoa wa Shinyanga inawashikilia watu wanne wanaodaiwa kufanya mauaji ya mama na mtoto wake baada ya kukodishwa kwa malipo ya Sh2.2 milioni.

 

Shinyanga. Jeshi la Polisi mkoa wa Shinyanga nchini Tanzania inawashikilia watu wanne wakiwemo ndugu watatu kwa tuhuma za mauaji ya Kalekwa Shiku (50) na mtoto wake Kuyonza Kubeja (30).

Watuhumiwa wanadaiwa kutekeleza mauaji hayo kati ya Juni 11 na Julai 18, 2019 kwa ahadi ya malipo ya Sh2.2 milioni.

Marehemu wote wawili, mama na mtoto wake walikuwa wakazi wa kijiji cha Mwampangabule wilaya ya Shinyanga.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Shinyanga, Richard Abwao aliwataja watuhumiwa wanaoshikiliwa kwa mauaji hayo yaliyotokea kati ya Juni 11 na Julai 18, 2019 kuwa ni pamoja na Jumanne Kwangu, Daniel Kwangu, Emmanuel Kwangu na Mihayo Ferdinand.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Jumapili Agosti 18, 2019, Kamanda Abwao amesema watuhumiwa hao wamekiri kuhusika na mauaji hayo baada ya kuahidiwa malipo ya Sh2.2 milioni.

Akifafanua Kamanda Abwao alisema watuhumiwa hao waliahidiwa Sh1 milioni kwa kumuua Shiku na Sh1.2 milioni iwapo wangefanikiwa kumuua Kubeja.

Alisema watuhumiwa Daniel Kwangu na Emmanuel Kwangu walimlaghai Kubeja ili waende naye mkoani Katavi kutafuta kazi na kufanikiwa kumuua Juni 11, 2019 na kutupa mwili wake ndani ya pori la mlima Kasanga.

“Agosti 8, 2019 askari polisi waliongozana na watuhumiwa hadi Mpanda mkoani Katavi na kufanikiwa kupata mabaki ya mwili wa binadamu yakiwemo mifupa, nywele na meno yanayoaminika kuwa ya Kubeja yakiwa yametupwa katika pori la mlipa Kasanga,” alisema Kamanda Abwao

Akizungumzia tukio la mauaji ya Shiku yaliyotokea Julai 18, 2019, Kamanda Abwao amesema watuhumiwa walifika nyumbani kwake na kumlaghai kuwa anaitwa na mmoja wa wazee kijijini hapo na kumuua kwa kumkata shingo kabla ya kufunga mwili wake kwenye mfuko wa sandarusi na kuutupa ndani ya bwawa la maji.

Upelelezi kuhusu matukio hayo unaendelea na watuhumiwa wanatarajiwa kufikishwa mahakamani kujibu mashtaka ya mauaji.