Mbatia azungumzia kauli ya Magufuli

Muktasari:

Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia amempongeza Rais wa Tanzania, John Magufuli baada ya kiongozi mkuu huyo wa nchi kusema uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 utakuwa wa amani, uhuru na haki.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia amempongeza Rais wa Tanzania, John Magufuli baada ya kiongozi mkuu huyo wa nchi kusema uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 utakuwa wa amani, uhuru na haki.

Mbatia ametoa kauli hiyo leo Jumatano Januari 22, 2020 baada ya kuulizwa na Mwananchi kuhusu kauli ya Magufuli aliyoitoa jana  Jumanne katika hafla ya chakula cha jioni aliyowaandalia mabalozi na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam.

Magufuli amesema shughuli ya uchaguzi ni muhimu kwa nchi yoyote inayofuata misingi ya kidemokrasia kama Tanzania, hivyo Serikali imejipanga kuhakikisha uchaguzi huo unafanyika katika mazingira ya amani.

Katika maelezo yake, Mbatia ambaye pia ni mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) amemtaka Rais Magufuli kutekeleza ndoto yake hiyo.

“Kuweka malengo bila kuyatekeleza ni ndoto za mchana na ukiwa unasema jambo bila kuwa na malengo ni kupoteza muda. Ukiwa na malengo na ukatenda inavyotakiwa utaleta mabadiliko chanya.”

“Naipongeza kauli ya Rais, ni kauli nzuri na ya inaleta  matumaini. Ni kauli ya kujenga umoja wa kitaifa kwa kuwa ametamka neno haki kuwe na uchaguzi huru na wa haki, ukipata haki unapata mshikamano,” amesema Mbatia.