Mbosso amlilia Boss Martha siku ya wapendanao

Friday February 14 2020

 

By Nasra Abdallah, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Msanii wa Bongofleva, Mbwana Yusufu maarufu  Mbosso  Khan ameitumia siku ya wapendanao leo Ijumaa Februari 14, 2020 kumkumbuka msanii wa kundi la vichekesho la Cheka Tu, Martha Michael ‘Boss Martha’ aliyefariki dunia Septemba, 2019.

Baada ya kifo cha Martha, msanii huyo wa kundi la WCB alisema kuwa waliwahi kuwa wapenzi na kupata mtoto mmoja kauli ambayo ilipingwa na baadhi ya ndugu wa Martha.

Leo Ijumaa Februari 14, 2020 katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram, Mbosso alimkumbuka mchekeshaji huyo kwa kuandika, “Dear Martha, dunia leo inasherehekea sikukuu ya wapendanao watu wana furaha sana huku duniani.”

“Rangi nyekundu na makopa mujarabu yametawala sana leo ..., ila kwangu ipo kinyume sana , kilichonitawala ni sura yako na ya mtoto wetu Ibrahim Mbwana Kilungi na nimeambiwa tu za chinichini siku hizi anaitwa Joseph , imani yangu inaniambia huko alipo yupo salama hivyo basi usiwe na shaka juu ya hilo.”

Ameongeza, “mwisho nikutoe hofu tu kuwa sasa nimeacha kulia mzee mwenzangu, najitahidi kuilazimisha furaha japo moyoni nina majonzi, na kibaya zaidi nashindwa kuanza maisha mapya pasi na upeo wako.”

"Kila siku nakuombea na nitazidi kukuombea roho yako iwe kwenye pepo ya Firdausi Inshaallah, pumzika Martha acha mimi niwasindikize wapendanao kwenye siku yao ya wapendanao.”

Advertisement

Advertisement