Mbowe, Lissu waongeza joto uchaguzi Chadema

Arusha/mikoani. Joto la uchaguzi wa Chadema limeshika kasi baada ya vigogo kuchukua fomu katika siku ya mwisho, huku Tundu Lissu akiingia rasmi kwenye kinyang’anyiro cha makamu mwenyekiti licha ya kuendelea kuwa ughaibuni.

Freeman Mbowe, ambaye ni mwenyekiti, Frederick Sumaye, ambaye ni mjumbe wa Kamati Kuu, walirejesha fomu za kuwania uenyekiti, huku Saed Kubenea, ambaye ni mbunge wa Ubungo, akijitosa kupambana na Lissu.

Wakati hayo yakiendelea, mjumbe mwingine wa Kamati Kuu aliyechukua fomu ya kuwania uenyekiti, Cecil Mwambe alianguka katika uchaguzi wa mwenyekiti wa Kanda ya Kusini, nafasi ambayo imekwenda kwa beki wa zamani wa soka, Seleman Mathew.

Mwambe amefuata njia ya Sumaye ambaye alianguka katika uchaguzi wa mwenyekiti wa Kanda ya Pwani ambayo alisimama peke yake.

Katika Kanda ya Kaskazini, Godbless Lema aliibuka mshindi wa nafasi ya mwenyekiti sawa na Ezekia Wenje katika Kanda ya Victoria.

Mgombea ambaye atavuta macho ya wengi ni Lissu, ambaye yuko nje ya nchi tangu Septemba 7, 2017 baada ya kushambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana akiwa nje ya makazi yake mjini Dodoma.

Lissu, ambaye alijaza fomu yake kimtandao, anawania nafasi ya makamu mwenyekiti, ambayo kwa sasa inashikiliwa na Profesa Abadalah Safari, ambaye alishasema aliomba kutogombea na kubaki mshauri wa chama.

Akizungumza kwa simu kutoka Ubelgiji, Lissu aliiambia Mwananchi kuwa hana tatizo na kugombea nafasi hiyo akiwa nje.

“Ninahitaji kufanya kampeni, ninahitaji kuomba kura, (lakini) kwa sababu ni mgombea inatosha kabisa,” alisema alipoulizwa atafanyaje kampeni akiwa nje ya nchi.

“Kuna maelfu ya wanachama wa chama changu ambao wanaweza kuniombea kura. Hoja kwamba nagombea ni taarifa kwamba naomba kura kwa hao wanaopiga kura.

“Wakitaka niseme nikiwa Ubelgiji nitasema, lakini wanafahamu msimamo wangu vya kutosha.” Akijibu swali kwa nini ameamua kugombea nafasi hiyo ilihali ni mwanasheria mkuu wa Chadema, Lissu aliyekuwa mbunge wa Singida Mashariki, alisema: “Nagombea nafasi ambayo naona nastahili. Kwangu kwa muda huu ni nafasi ya makamu mwenyekiti wa chama.

“Mwanasheria mkuu wa chama ni nafasi muhimu sana, si nafasi ya kisiasa sana bali nafasi ya kiutendaji. Katika hatua nilipo, nafikiri nahitaji kuchangia kama mjumbe wa chama kama mjumbe wa Kamati Kuu na kadhalika. Ndiyo maana nimeshauriana na viongozi wenzangu kwanza.”

Jana, akifungua mkutano wa Baraza la Uongozi la Chadema Kanda ya Kaskazini, Mbowe alisema alimuomba Lissu agombee naye akakubali.

Alisema Lissu alisaini fomu hizo hivi karibuni akiwa Nairobi, Kenya na kuwataka wagombea wa nafasi nyingine kuwa na nidhamu ya uongozi kwa kuacha kutoa lugha chafu mitandaoni.

Katika nafasi hiyo atapambana na Kubenea ambaye pamoja na Anthony Komu (Moshi Vijijini) wamepelekwa kamati ya nidhamu baada ya sauti zao kusambaa mitandaoni wakizungumzia viongozi wa chama hicho.

Lakini Kubenea alisema amejipanga kumkabili Lissu.

“Nimejipanga kukabiliana naye. Demokrasia itaamua kwa kuwa na mimi nina wajibu wa kuongoza hiki chama ili kufanya mageuzi katika hii nchi,” alisema.

Tofauti na uchaguzi uliopita Septemba mwaka 2014, uchaguzi wa mwaka huu unaonekana kuwa na mvutano kuanzia ngazi za Kanda pamoja na taifa hasa kutokana na majina ya wagombea.

Sumaye alirejesha fomu jana na baadaye kuiambia Mwananchi kuwa amejaza na kurejesha fomu na sasa “nasubiri mchakato unaofuata”.

Alipoulizwa kuhusu mchuano kwenye nafasi hiyo na nyingine ambako vigogo wanachuana, Sumaye alisema haoni kitu cha ajabu.

Mbowe alichukuliwa fomu hizo na kundi la vijana wa Chaderma ambao jana walimpa azisaini na baadaye kuzirejesha.

“Nilikusudia kutokuwa kiongozi Chadema si kwa woga bali ni dhamira ya kuwapa wengine nafasi ya wagombea kama sheria na katiba ya chama inavyosema. Lakini wameniomba kuwa tena mwenyekiti wa Taifa na baada ya kunichukulia fomu, nimekubali,” alisema Mbowe.

Katika mkutano huo uliokuwa unalenga kuchagua viongozi wa kanda hiyo, Mbowe iliwataka wanachama na madiwani Chadema kutowaona wasaliti wanaohama chama hicho kwa kuwa kuwa mpinzani unakabiliwa na changamoto nyingi ambazo zinahitaji uvumilivu mkubwa.

Pia, aliwaonya baadhi ya wanachama wanaotumia mitandao vibaya kuchafua viongozi na kwamba watawashughulikia kwa kufuata sheria na katiba.

Kuhusu jimbo lake la Hai, Mbowe aliwaomba radhi wanachama na wakazi wa Hai kwa kutoonekana mara kwa mara, akisema anabanwa na majukumu.