Mbowe: Tumepata somo, hatuna haraka ya kumpokea Membe

Muktasari:

Asema wamepata somo kubwa la kuwapokea wanachama wa CCM wasio na malengo ya muda mrefu na Chadema.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema chama hicho kimepata somo kuwapokea wanachama wapya  kutoka CCM aliodai kuwa hawana malengo ya muda mrefu, wanajali zaidi maslahi yao.

Akizungumza leo Alhamisi Machi 5, 2020 katika kipindi cha Jahazi cha Redio Clouds, Mbowe ambaye hakutaka kuingia kwa undani kuhusu aliyekuwa mwanachama wa CCM, Bernard Membe, kusema kwa sasa chama hicho kitakuwa makini.

Membe aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje katika Serikali ya Awamu ya Nne amefukuzwa uanachama wa CCM kwa madai ya kukiuka maadili ya chama hicho.

Mawaziri wakuu wa zamani, Edward Lowassa na Frederick Sumaye ni miongoni mwa waliojiunga na  Chadema wakitokea CCM mwaka 2015 lakini wamerejea tena katika chama hicho tawala.

“Nisingependa kuingia kwenye mjadala wa Membe kwa sababu yeye ni Mtanzania ana haki ya kujiunga na chama chetu, akiona kinakidhi matamanio yake ya kiitikadi, sasa mimi hilo sijui kwa sababu sijui misimamo yake ya kiitikadi,” amesema Mbowe.

Mbowe ametoa kauli hiyo wakati Chadema ikiugulia maumivu ya kuondokewa na makada wake waliohama kutoka CCM na sasa wamerudi walikotoka kwa madai ya kuunga mkono juhudi za Serikali.

“Nisiwe mpiga ramli kwamba labda labda, lakini tutakuwa waangalifu sana kupokea wanachama waliotoka kwenye vyama vingine vya siasa kutokana na experience (uzoefu) tuliyopata kwa miaka michache iliyopita.”

“Kwamba watu wanahama vyama si kwa sababu wanaamini katika mnachokiamini, ila wanaona kuna maslahi fulani, sasa hatuwezi kuongozwa na masilahi, lazima tuongozwe na malengo ya kikatiba,” amesema Mbowe.

Ameendelea kusisitiza kuwa chama hicho kimepata funzo kupokea wanachama kutoka CCM wasio na malengo ya muda mrefu ya chama hicho.  

“Tuna experience kwa mwaka 2015 hadi 2020 kubeba wanachama ambao hawaamini katika itikadi yenu, hawaamini katika malengo yenu lakini wanaangalia maslahi yao ya muda mfupi. Tuna experience hali hiyo na nikiri kuwa yametupa somo la kutosha.”

“Kwa hiyo hatuna haraka ya kumpokea kada yoyote wa chama cha siasa. Hatuna sababu ya kumkatalia mtu lakini tunaweza kumpokea mtu tukamweka katika uangalizi, yapo mambo mengi yanaweza kuzungumzika kutokana na haiba ya mtu,” amesema.