MPYA: Mbowe, wenzake washindwa kulipa faini Sh350 milioni, kulala rumande

Muktasari:

Viongozi wanane wa Chadema akiwemo mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe wamepelekwa katika gereza la Segerea kutokana na kushindwa kulipa faini ya Sh350 milioni.

Dar es Salaam. Viongozi wanane wa Chadema akiwemo mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe wamepelekwa katika gereza la Segerea kutokana na kushindwa kulipa faini ya Sh350 milioni.

Ni baada ya mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwatia hatiani katika mashtaka 12 katika ya 13 yaliyokuwa yanawakabili na kutakiwa kulipa faini hiyo lakini wameshindwa.

Wakati wanatoka mahakamani hapo waliwasalimu wafuasi wa chama hicho waliokuwa nje ya uzio wa mahakama hiyo na kuanza kuwashangilia. Waliondoka mahakamani hapo wakiwa wamepanda gari tatu za polisi aina ya Landcruiser.

Jopo la mawakili wa washtakiwa hao wakiongozwa na Peter Kibatala wamesema wanakata rufaa kupinga hukumu hiyo.

Uamuzi wa kuwatia hatiani umetolewa leo Jumanne Machi 10, 2020 na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama  hiyo, Thomas Simba baada ya kupitia ushahidi wa upande  wa mashtaka na ule wa utetezi.

Mbali na Mbowe na Dk Mashinji, washtakiwa wengine ni Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika; Naibu Katibu Mkuu Salum Mwalimu (Zanzibar), Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa.
Pia wamo mbunge wa Tarime mjini, Esther Matiko; mbunge wa Kawe, Halima Mdee; mbunge wa Bunda, Esther Bulaya na mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche.