Mbowe amjibu Ndugai kuhusu utoro bungeni

Muktasari:

Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe amemjibu Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai aliyedai kuwa mbunge huyo wa Hai ni mtoro bungeni.

Dar es Salaam.  Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe amemjibu Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai aliyedai kuwa mbunge huyo wa Hai ni mtoro bungeni.

Akizungumza na Mwananchi leo Ijumaa Novemba 15, 2019  Mbowe amesema yeye pamoja na wabunge wengine sita wa chama hicho hawapo bungeni kwa kuwa wanahudhuria kesi inayowakabili katika mahakama ya hakimu mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam.

Jana Alhamisi Novemba 14, 2019 bungeni mjini Dodoma, Ndugai alisema kambi hiyo inakosa nafasi za mara kwa mara kuuliza maswali kwa Waziri Mkuu kwa sababu ya utoro wa Mbowe.

Amesema katika kipindi hicho swali la kwanza huulizwa na kiongozi wa kambi hiyo.

“Bunge linaendelea na vikao bungeni na huku  mahakama inaendelea kusikiliza kesi inayotukabili sasa anategemea ni mbunge gani atakuwepo kila mahali kwani mimi nimekuwa mchawi huku niwepo na kule niwepo,” amesema Mbowe.

Mbowe na viongozi wengine wanane wa Chadema kwa pamoja wanakabiliwa na  mashtaka 13, ikiwemo kula njama, kufanya mkusanyiko wenye ghasia na kuhamasisha hisia za chuki.

Pia, wanadaiwa kushawishi hali ya kutoridhika, uchochezi wa makosa yanayodaiwa kutendeka kati ya Februari 1 na 16, 2018, jijini Dar es Salaam.

Mbali na Mbowe wengine ni mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche;  Mchungaji Peter Msigwa (Iringa Mjini), Halima Mdee (Kawe) na Ester Bulaya (Bunda).

Esther Matiko (Tarime Mjini); katibu mkuu wa chama hicho, Dk Vicent Mashinji na naibu makatibu wakuu, Salum Mwalimu (Zanzibar) na John Mnyika (Bara).

Kwa habari zaidi fuatilia gazeti la Mwananchi la kesho Jumamosi Novemba 16, 2019