Mbunge CUF ahoji hatima ya jimbo lake

Mbunge wa Mchinga (CUF), Hamidu Bobali

Muktasari:

Mbunge wa Mchinga (CUF), Hamidu Bobali amehoji hatma ya jimbo hilo baada ya Rais wa Tanzania, John Magufuli kufanya marekebisho ya jina na mipaka ya iliyokuwa Halmashauri ya Wilaya ya Lindi na kuanzisha Halmashauri mpya ya Mtama inayojumuisha eneo lote la jimbo la Mtama.

Dodoma. Mbunge wa Mchinga (CUF), Hamidu Bobali amehoji hatma ya jimbo hilo baada ya Rais wa Tanzania, John Magufuli kufanya marekebisho ya jina na mipaka ya iliyokuwa Halmashauri ya Wilaya ya Lindi na kuanzisha Halmashauri mpya ya Mtama inayojumuisha eneo lote la jimbo la Mtama.

“Je nini hatma ya eneo lililobaki la jimbo la Mchinga ambalo hapo awali ilikuwa ipo ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Lindi kama ilivyo kwa Jimbo la Mtama,” amehoji.

Akijibu swali hilo, Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo amesema kufuatia agizo la Rais Magufuli, ofisi yake inaendelea na uhakiki wa mipaka ili kuandaa tangazo la Serikali la kurekebisha mipaka ya halmashauri hizo.

“ Zoezi hilo linafanyika sambamba na maeneo mengine yaliyotangazwa na Rais ili kuboresha utoaji huduma kwa wananchi,” amesema.