VIDEO: Mbunge Chadema atoa sababu ya kutaka kumrithi Mbowe

Muktasari:

  • Chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania cha Chadema kitafanya uchaguzi wa kupata viongozi Desemba 18, 2019 ambapo sasa shughuli ya uchukuaji na urejeshaji wa fomu unaendelea na utahitimishwa Novemba 30, 2019.

Dar es Salaam. Mbunge wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania cha Chadema, Cecil Mwambe amesema anagombea nafasi ya juu ya chama hicho ili kumsaidia mwenyekiti wa sasa, Freeman Mbowe ‘ambaye kama binadamu amechoka.”

Mwambe ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema amesema hayo leo Jumanne Novemba 26, 2019 alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu adhima ya kugombea nafasi hiyo.

Amesema anajua Mbowe amefanya mengi ila kama binadamu huchoka na kuhitaji usaidizi hivyo ameamua kujitokeza kumsaidia.

"Niwashukuru wale wote walioniunga mkono licha ya masimango na matusi waliyoelekezewa," amesema Mwambe.

Amesema uchaguzi usio na ushindani hutoa viongozi ambao mwisho wa siku hudai kwanza sikutaka au nilishurutishwa.

Mbunge huyo amesema alianza kuona haja ya kugombea baada ya kumshuhudia Mbowe ambaye ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni akitishia kuachia nafasi hiyo kwa zaidi ya mara tatu.

"Nikaona ipo haja ya kumpokea kijiti hasa baada ya kueleza kwa kina madhila ambayo amepitia kwa vipindi vilivyopita," amesema Mwambe ambae pia ni Mwenyekiti wa Kanda ya Kusini ya chama hicho aliyepitishwa tena kugombea nafasi hiyo

Amesema anachotaka ni viongozi kuelewa kuwa uongozi ni dhamana ambayo mtu akiomba na kupewa ni lazima aithamini jambo ambalo atafanya.

Mwambe amesema anataka nafasi hiyo ili kuimarisha zaidi ngazi za chini za chama hicho.

"Ninao mtazamo kuwa uzito unaotolewa sasa kwa ngazi ya mikoa, wilaya na majimbo ni mdogo kulingana na umuhimu wa ngazi hizi," amesema Mwambe ambaye tayari amekwisha kuchukua fomu na kudai leo Jumanne anairejesha makao makuu ya chama hicho, Kinondoni jijini Dar es Salaam.

Jana Jumatatu, baadhi ya vijana wa Chadema walijitokeza makao makuu ya chama hicho kumchukulia fomu Mbowe wakisema watakwenda kesho Jumatano kumshawishi ili agombee tena nafasi hiyo.