Mbunge Lwakatare aaga bungeni

Mbunge wa Bukoba Mjini (Chadema), Wilfred Lwatare akichangia mjadala wa Hotuba ya Ofisi ya Rais, Tawala na Serikali za Mitaa kwa Mwaka wa Fedha, 2020/2021 bungeni jijini Dodoma leo. Picha na Anthony Siame

Muktasari:

Mbunge wa Bukoba Mjini, Wilfred Lwakatale ameaga bungeni akimtakia mafanikio zaidi atakayeshika nafasi hiyo afanye vizuri zaidi yake lakini amejivunia kuondoka bila madeni

Dodoma. Mbunge wa Bukoba Mjini nchini Tanzania, Wilfred Lwakatare (Chadema) ameaga rasmi bungeni kuwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka uu hatagombea ubunge badala yake anawatakia mafanikio wengine.
Lwakatare ametoa kauli hiyo leo Jumanne Aprili 14,2020 ndani ya Bunge wakati akichangia hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi katika Ofisi ya Rais (Tamisemi) ambapo ametaja mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha uongozi wake akijivunia kuwa kiongozi wa kambi ya upinzani wa kwanza katika mfumo wa vyama vingi nchini Tanzania.
Katika hotuba yake wakati akichangia, amesema katika utumishi wake alianzia kufanya kazi Tamisemi kabla ya kugombea nafasi ya mwenyekiti wa mtaa nafasi iliyompa jeuri ya kugombea ubunge akiwa upinzani katika chama cha Cuf ambapo alishinda.
Tofauti na siku zote, leo alikuwa akichangia kwa upole na taratibu amesema kwenye maisha yake anaondoka ubunge akijivunia mambo mengi ikiwemo ushirikiano mkubwa aliokuwa anapewa na madiwani wa vyama vyote katika halmashauri ya wilaya ya Bukoba pamoja na watumishi wote.
“Najivunia sana kuwa upinzani na kuuimarisha upinzani katika kipindi chote nilichokuwa mbunge na ndani ya upinzani, naondoka nikiwa na furaha na amani nikiomba mbunge atakayekuja baada yangu aendeleze mafanikio haya,” amesema Lwakatare.
Lwakate alianza kwa kushukuru kwamba yeye ni miongoni mwa wabunge wasiokuwa na madeni hivyo hana mashaka katika kupumzika kwake katika siasa kwa kuwa kama ni kiinua mgongo atapata bila hofu.
Hata hivyo hakusema kama hatajihusisha ndani ya siasa au ataendelea kuwa mwanasiasa katika nafasi zingine lakini Naibu Spika Dk Tulia Akson amemkumbusha kuwa wapo wengine huwa wanaaga ndani ya bunge lakini ukifika wakai huchukua fomu na kugombea.