Mbunge ahoji hisa za Z’bar ATCL

Muktasari:

Mbunge wa Mwanakwerekwe (CUF), Ali Salim Khamis ameitaka serikali kutoa mchanganuo wa hisa ngapi zinamilikiwa na Zanzibar kwenye Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL).

Dodoma. Mbunge wa Mwanakwerekwe (CUF), Ali Salim Khamis ameitaka serikali kutoa mchanganuo wa hisa ngapi zinamilikiwa na Zanzibar kwenye Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL).

Khamisi alitoa hoja hiyo akihoji sababu za mambo hayo kutowekwa hadharani kama ilivyo kwa Benki Kuu ambayo Zanzibar inamiliki hisa 12.

Katika swali la msingi mbunge huyo alitaka kujua iwapo ATCL ni shirika la Muungano na lini ATCL italipa deni la kodi ya kutua (landing fee) kwa Mamlaka ya Anga ya Zanzibar.

Kwa upande wake, mbunge wa Kasulu Mjini, Daniel Nsanzugwako ameitaka Serikali kuangalia upya jinsi ya kuajiri watumishi kwa kuwa ATCL ina wafanyakazi zaidi ya 200 wakati ina ndege moja.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Edwin Ngonyani amesema ATC inamilikiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano kwa asilimia 100.

Ngonyani amesema umiliki wa ATCL haujatenganishwa kuonyesha asilimia za hisa zinazomilikiwa na serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano.