Mchungaji awataka wazazi kushirikiana na walimu katika maswala ya maadili

Wahitimu wa darasa la saba shule ya msingi Heritage.

Dar es salaam. Wazazi wametakiwa  kushirikiana na walimu katika kuwafundisha watoto maadili na  kujitegemea badala yakuangalia ufaulu peke yake.

Hayo yamesemwa leo Septemba 29,2019 na Mchungaji wa Kanisa la Adventista Wasabato jimbo la kusini mashariki Steven Ngusa wakati wa mahafali ya 12 ya darasa la saba shule ya msingi Heritage iliyoko Ilala.

Amesema mtoto anapopelekwa shule jukumu la malezi limekuwa likibaki kwa walimu kitendo kinachosababisha wanashindwa kuwa na maadili yakutosha.

"Unapompeleka mtoto shule usibaki kuangalia tu ufaulu shirikianeni na walimu kufuatilia mambo mengine ikiwemo maadili yao"Amesema Mchungaji Ngusa

Amesema jambo lingine wazazi wanalopaswa kufanya na kulizingatia nikuwafundisha watoto kujitegemea na kufanya kazi badala yakuwaacha huru kila wakati.

"Hata uwe tajiri lazima kuwafundisha watoto kufanya kazi nakujitegemea jambo hilo litasaidia kujiepusha na makundi yasiyofaa"ameongeza

Mkuu wa shule hiyo Magabe Kimori  amewataka wanafunzi waliohitimu kuzingatia maadili waliofundishwa na kuwa na nidhamu shule watakazokwenda kuendelea kidato cha kwanza.

"Shule hii inafundisha kwa vitendo lakini kikubwa ni nidhamu kwa wanafunzi tunatamani yote tunayoyafundisha wakayaendeleze huko waendako" amesema Mkuu wa shule Kimori.

Akiongea kwa niaba ya wahitimu Bestina Lyamunda amesema mafanikio waliyoyapata yametokana na kusoma kwa bidii huku wakijituma na kumwomba Mungu .

Katika mahafali hayo jumla ya wanafunzi 103 wa darasa la saba  wamehitimu na kukabidhiwa vyeti.