Mchungaji mbaroni, adaiwa kukutwa na meno ya tembo

Muktasari:

Watu watatu akiwamo mchungaji wa Kanisa la Anglikana wanashikiliwa na Polisi Mkoani Dodoma kwa tuhuma za kukutwa na nyara za Serikali (meno ya tembo).

Dodoma. Mchungaji wa Kanisa la Anglikana kijiji cha Chinyika wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma, Sekandi Mkombola (44) anashikiliwa na polisi akituhumiwa kukutwa na meno ya tembo mawili yenye uzito wa kilo 15.

Kamanda wa polisi mkoani Dodoma, Gilles Muroto leo Jumatatu Novemba 4,2019 amesema mchungaji huyo alikamatwa Oktoba 26, mwaka huu akisafirisha meno hayo kwa pikipiki kutoka Mungui kwenda Pwaga.

Muroto amesema  zipo taarifa za washiriki wengine katika uhalifu huo ambao wanawafuatalia ili wawakamate.

 “Niwaagize wajisalimishe haraka, wasalimishe na silaha wanazotumia katika uhalifu huo kwa kuwa msako dhidi yao ni mkali, watakamatwa popote watakapokuwa,” amesema Muroto.

Katika tukio lingine polisi mkoani Dodoma  jana Novemba 3, 2019 katika eneo la Stendi Kuu ya mabasi Nanenane, limewakamata watuhumiwa wawili wanaume wakiwa na vipande 16 vilivyokatwa katwa sawa na meno sita ya tembo watatu.

Muroto amesema mbinu waliyotumia kusafirishia ni kukata dumu la lita 20 juu kisha kuvitumbukiza vipande hivyo vikiwa ndani ya mfuko.

Amesema majina ya watuhumiwa yamehifadhiwa na uchunguzi zaidi unaendelea ili kuwakata washiriki wengine pamoja na silaha zilizotumika kwenye tukio hilo.