Membe: Bila uhuru wa vyombo vya habari, serikali itakuwa dumavu

Aliyekuwa waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania, Bernard Membe

Muktasari:

Mwili wa mwili wa mwandishi wa habari nchini Tanzania, Godfrey Dilunga (43) umeagwa leo Alhamisi katika viwanja vya Mnazi mmoja, Dar es Salaam kisha utasafirishwa kwenda mkoani Morogoro kwa mazishi yatakayofanyika kesho Ijumaa.

Dar es salaam. Aliyekuwa waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania, Bernard Membe amesema Serikali inaweza kuwa  dumavu endapo haitaruhusu uhuru wa vyombo vya habari Tanzania.

Membe ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Septemba 19, 2019 wakati shughuli ya kuaga mwili wa mwandishi wa habari nchini Tanzania, Godfrey Dilunga (43) katika viwanja vya Mnazi mmoja, Dar es Salaam na kuhudhuriwa na wanahabari, viongozi wa serikali, pamoja na wanasiasa mbalimbali.

Dilunga aliyefariki dunia Septemba 17, 2019 katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Dar es Salaam alipokuwa amelazwa kwa matibabu ya homa ya tumbo.

Akitoa salamu zake za rambirambi mbele ya wanahabari hao, Membe amesema Dilunga ameondoka akiwa anastahili heshima ya Taifa kupitia kazi yake ya uandishi wa habari.

"Siku hii tunapomuaga Dilunga, itukumbushe uhuru wa vyombo vya habari, kazi ya uandishi wa habari ni sawa na mbolea, unapoiweka katika mche inachipua."

"Bila kazi ya vyombo vya habari, serikali itakuwa dumavu, vyama vya siasa havitakuwa na afya," amesema Membe

Membe amesema afya ya serikali na vyama vya siasa inatokana na mchango wa vyombo vya habari duniani.

"Dilunga alishiriki mikutano yangu yote ya waandishi nikiwa waziri wa mambo ya nje na ushirikiano wa Afrika mashariki," amesema Membe.

"Hata nilipomaliza muda wangu bado tuliendelea kuwasiliana. Dilunga niliyemfahamu alikuwa na msimamo, ametuachia fundisho."

Mwanasiasa huyo amesema, "kwa kweli tumempoteza mwandishi tegemezi, shujaa, jambo la msingi tuwe huru kuandika habari bila woga ili nchi yetu iendelee."