Meneja Tanroad arudishwa wizarani kwa kushindwa kukagua madaraja

Muktasari:

  • Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameagiza Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroad) Mkoa wa Morogoro,  Godwin Andalwisye arejeshwe wizarani na nafasi yake ijazwe na mtu mwingine  baada ya kuzembea kutimiza wajibu wake.

Morogoro. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameagiza Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroad) Mkoa wa Morogoro,  Godwin Andalwisye arejeshwe wizarani na nafasi yake ijazwe na mtu mwingine  baada ya kuzembea kutimiza wajibu wake.

Uamuzi huo umekuja baada ya kiongozi huyo kushindwa kufanya ukaguzi wa usalama wa madaraja yaliyoko kwenye mkoa wake na kubaini kama kuna daraja lina matatizo hali iliyosababisha daraja la Kiyegea lililopo eneo la Gairo linalounganisha Mkoa wa Morogoro na Dodoma kuvunjika.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo Jumatano Machi 4, 2020 baada ya kutembelea eneo hilo na kukagua ukarabati ili kurejesha mawasiliano ya barabara.

Waziri Mkuu ameshuhudia mrundikano wa magari na abiria hali ambayo haikumfurahisha.

“Hivi unajua udhahifu wako ni kwa sababu hukufanya ukaguzi kuona kama daraja limejaa mchanga au uchafu ambao umesababisha kipenyo cha kupitisha maji kuwa kidogo na maji yakalazimika kupanda juu hali ambayo ilisababisha daraja hili kusombwa na maji,” amesema.

Amesema wakati njia hiyo inarekebishwa itengenezwe njia nyingine ya muda ili kuweza kupitisha magari na kisha Serikali itachukua hatua baada ya kubaini nini kimesababisha. 

Ili kuharakisha kazi hiyo inakamilika kwa haraka, Waziri Mkuu ameagiza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano,  Isack Kamwelwe, Katibu Mkuu wa wizara hiyo pamoja na wahandisi wote wa Tanroad Mkoa wa Morogoro na Dodoma leo wakutane kwenye eneo la tukio na wahakikishe kuanzia kesho Alhamisi njia hiyo iwe imefunguka.

Majaliwa amesema atawasiliana na Mkuu wa Majeshi CDF Jenerali Venance Mabeyo ili aweze kupata msaada wa wanajeshi  kuongeza nguvu  kuhakikisha mawasiliano yanarejea haraka.