VIDEO: Mfanyabiashara aliyegoma kuwapa rushwa TRA afunguka

Mfanyabiashara Ramadhani Ntunzwe 

Muktasari:

Jana Ijumaa Juni 7, 2019 Rais wa Tanzania, John Magufuli alimwagiza Kamishna Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Diwani Athuman kuwakamata na kuwafikisha mahakamani watumishi watatu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa tuhuma za kuomba rushwa kutoka kwa mfanyabiashara, Ramadhani Ntunzwe wa Kariakoo jijini Dar es Salaam


Dar es Salaam. Mfanyabiashara Ramadhani Ntunzwe aliyetajwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuwa miongoni mwa wafanyabiashara waliosumbuliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kuchukuliwa mizigo yake kwa zaidi ya miaka mitatu, ameeleza kwa kina mkasa aliompata.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumamosi Juni 8, 2019, mbali na mali zake hizo alizonunua nchini Afrika Kusini, Ntunzwe amedai kusababishiwa hasara ya mamilioni ya fedha kutokana na mazigo wake kushikiliwa na TRA tangu mwaka 2016 hadi Machi 2019.

Sakata hilo lilitua jana Ijumaa Ikulu jijini Dar es Salaam katika mkutano wa Rais John Magufuli na wafanyabiashara watano kutoka kila wilaya nchini ambapo Majaliwa wakati akizungumzia malalamiko dhidi ya TRA yaliyotolewa na wafanyabiashara hao aligusia mkasa huo wa Ntunzwe.

Baada ya kueleza suala hilo Rais Magufuli alitoa maagizo kwa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) kuwakamata wahusika wote wa sakata hilo ambao ni watumishi watatu wa TRA na kuwapeleka mahakamani.

Pia, Rais Magufuli aliagiza TRA ifanye tathimini ya hasara aliyoipata mfanyabiashara huyo kwa kushikilia mali zake na imlipe.

Ntunzwe amesema alinunua mzigo huo nchini Afrika Kusini na kuupitishia katika mpaka wa Tunduma Oktoba 2016 lakini ulikuja kushikiliwa na TRA hadi Machi 2019, huku pia mamlaka hiyo ikilifunga duka lake lililopo mtaa wa Congo jijini Dar es Salaam na kumsababishia upotevu wa mali zenye thamani ya mamilioni.

Katika mahojiano na Mwananchi mfanyabiashara huyo ameelezea mkasa ulivyokuwa, jinsi alivyokwepa kutoa rushwa na waziri mkuu alivyomsaidia kupata mizigo mali zake.

Lakini hasara kiasi gani? Haya na mengine mengi usikose Gazeti la Mwananchi kesho Jumapili Juni 9, 2019.