Mfanyabiashara wa mafuta kuilipa Serikali ya Tanzania Sh8 bilioni

Muktasari:

  • Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemhukumu mfanyabiashara wa mafuta ya Petroli, Abshir Afrah (56) kulipa fidia ya Sh8.1 bilioni baada ya kumtia hatiani kwa kuisababishia hasara Serikali ya Tanzania.

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imemhukumu mfanyabiashara wa mafuta ya Petroli, Abshir Afrah (56) kulipa fidia ya Sh8.1 bilioni baada ya kumtia hatiani kwa kuisababishia hasara Serikali ya Tanzania.

Pia, ameamriwa na mahakama hiyo kutofanya kosa lolote linalofanana ndani ya kipindi cha miezi 12 kuanzia leo Alhamisi Novemba 14, 2019.

Afrah, mkazi wa Nairobi nchini Kenya na raia wa Somalia alikuwa akikabiliwa  na mashtaka ya kuisababishia hasara ya kiasi hicho cha fedha Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Hukumu hiyo imetolewa na Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo, Janeth Mtega baada ya mshtakiwa kutiwa hatiani kwa kosa la kuisababishia hasara Serikali.

Mshtakiwa alimuandikia barua mkurugenzi wa mashtaka nchini (DPP) kukiri na kuomba msamaha kuhusu mashtaka yanayomkabili.

Amelipa Sh800 milioni kama moja ya masharti waliyofikiana baina yake na DPP.

Ametakiwa kulipa Sh800 milioni na Sh7.2 bilioni zilizobaki akitakiwa kuzilipa ndani ya miezi 12.