Mgodi wa GGM kutumia Sh9.2 bilioni kwa miradi ya maendeleo

Viongozi wa halmashauri za Geita mji na Geita wilaya wakatiliana Saini na uongozi wa mgodi wa GGML hati ya makubaliano na halmashauri mbili za wilaya ya Geita kuashiria mwanzo wa utekelezaji wa miradi ya jamii kwa mwaka 2019

Muktasari:

Kampuni ya madini ya dhahabu ya Geita (GGM) imejipanga kutumia Sh9.2 bilioni mwaka wa fedha 2019/20  kutekeleza miradi ya maendeleo kwa wananchi wanaoishi karibu na mgodi huo

Geita. Kampuni ya madini ya dhahabu ya Geita (GGM) imejipanga kutumia Sh9.2 bilioni mwaka wa fedha 2019/20  kutekeleza miradi ya maendeleo kwa wananchi wanaoishi karibu na mgodi huo.

Kauli hiyo imetolewa na mkurugenzi mkuu wa kampuni hiyo, Richard Jordinson katika hafla ya kutiliana saini hati ya makubaliano na halmashauri mbili za wilaya ya Geita.

Amesema fedha hizo zitatumika kutekeleza miradi ya afya, mazingira, elimu, kilimo na miundombinu.

Amesema mgodi huo unaamini kufanya kazi pamoja na jamii inayowazunguka ili kuwa na uwajibikaji wa pamoja katika kutekeleza na kuitunza miradi ya maendeleo.

Akizungumza katika hafla hiyo mkuu wa Mkoa wa Geita,  Robert Gabriel amesema GGM ni kampuni ya kwanza iliyotii agizo la Serikali  linalozielekeza kampuni za madini kuandaa mpango unaoaminika wa uwajibikaji  jamii (CSR).

Gabriel amesema mapato yatokanayo na mgodi yameisaidia halmashauri ya mji kuongoza kwa mapato wa kukusanya kwa asilimia 157 na kuifanya kuwa miongoni mwa halmashauri tano zilizopeleka mapato yake kwenye miradi ya maendeleo kwa wananchi.

Amesema halmashauri mbili za wilaya ya Geita kwa mwaka wa fedha ulioisha zimechangia mapato ya mkoa kwa asilimia 62