Mgonjwa akwamisha kesi ya Zitto

Muktasari:

  • Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeshindwa kusikiliza ushahidi wa upande wa mashtaka katika kesi ya uchochezi inayomkabili mbunge wa Kigoma Mjini (ACT- Wazalendo), Zitto Kabwe kutokana na shahidi kuwa mgonjwa

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeshindwa kusikiliza ushahidi wa upande wa mashtaka katika kesi ya uchochezi inayomkabili mbunge wa Kigoma Mjini (ACT- Wazalendo), Zitto Kabwe kutokana na shahidi kuwa mgonjwa.

Hayo yameelezwa leo Ijumaa Novemba 22, 2019 na wakili wa Serikali mkuu, Tumaini Kweka akisaidiana na wakili wa Serikali mwandamizi, Nassoro Katuga.

Kweka amedai mbele ya hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi kuwa shahidi huyo anaumwa na leo ameshindwa kufika mahakamani hapo, kuomba tarehe nyingine kwa ajili ya kuendelea na ushahidi.

Hakimu Shaidi baada ya kusikiliza hoja hiyo ameahirisha kesi hiyo hadi Desemba 3, 2019.

Zitto anatetewa na wakili Jebra Kambole, Peter Kibatala na Steven Mwakibolwa.

Tayari mashahidi 14 wa upande wa mashtaka wameshatoa ushahidi wao

Katika kesi ya msingi, Zitto akabiliwa na mashtaka matatu yote ya uchochezi.

Mshtakiwa huyo anadaiwa kutenda makosa hayo, Oktoba 28, 2018 katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika ofisi za makao makuu ya chama cha ACT Wazalendo.

Katika shtaka la kwanza, anadaiwa kuwa siku hiyo akiwa katika mkutano na waandishi wa habari kwa nia ya kuleta chuki  miongoni mwa wananchi wa Tanzania dhidi ya Jeshi la polisi alitoa maneno ya uchochezi.

Anadaiwa kutoa maneno ya uchochezi kuwa, "watu ambao walikuwa ni majeruhi katika tukio la mapambano baina ya wananchi na polisi, wakiwa wamekwenda hospitali kupata matibabu katika kituo cha afya cha Nguruka, polisi walipata taarifa kuwa kuna watu wanne wamekwenda hospitali kituo cha afya Nguruka kupata Matibabu wakawafuata kule wakaua."