Mgonjwa wa kwanza wa corona Tanzania apona

Waziri wa Afya nchini Tanzania, Ummy Mwalimu

Muktasari:

  • Waziri wa Afya nchini Tanzania, Ummy Mwalimu amesema mgonjwa wa kwanza nchini wa virusi vya corona, Isabela Mwampamba (46) ameshapona ugonjwa huo na mpaka sasa wasafiri 245 wametengwa kwenye vituo vilivyoandaliwa baada ya kuingia nchini wakitoka nchi zilizoathirika zaidi na virusi hivyo.

Dar es Salaam.  Waziri wa Afya nchini Tanzania, Ummy Mwalimu amesema mgonjwa wa kwanza nchini wa virusi vya corona, Isabela Mwampamba (46) ameshapona ugonjwa huo.
Waziri Ummy amesema hayo leo Alhamisi Machi 26, 2020 jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Amesema kuwa baada ya Isabela kupitia vipimo vyote vimeonyesha kuwa amepona maambukizi hayo ya virusi vya corona.
Machi 16, mwaka huu Waziri Ummy alimtangaza Isabela kuwa mgonjwa wa kwanza wa corona ambaye aliwasili nchini akitokea Ubelgiji
Baada ya Isabela kugundulika kuwa na maambukizi ya ugonjwa huo, alitengwa karantini na Serikali iliendelea kuwafuatilia watu wote wa karibu ili kubaini hali zao.
Pia, Waziri Ummy amesema katika kuhakikisha kudhibiti maambukizi ya corona, mpaka jana Jumatano usiku jumla ya wasafiri 245 walioingia nchini kutoka nchi zenye maambukizi ya virusi vya corona wametengwa kwenye karantini za lazima kwa siku 14 kwa gharama zao.
“Kuanzia tarehe 23 hadi jana usiku (Jumatano) wasafiri 111 wametengwa katika vituo vilivyoandaliwa kwa Tanzania Bara na Zanzibar ni watu 134 na wenyewe wapo karantini,” amesema Ummy.
Amesema watu hao sio washukiwa wala wagonjwa wa corona bali wako chini ya uangalizi kutokana na kuingia nchini kutoka katika mataifa ambayo yameathirika zaidi.