VIDEO: Mhagama: Miradi 107 ya maendeleo ina kasoro

Muktasari:

Imeelezwa kuwa katika mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2019 miradi  107 ya maendeleo ya Sh90.2 bilioni kwenye halmashauri 82 nchini ina kasoro.


Lindi. Imeelezwa kuwa katika mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2019 miradi  107 ya maendeleo ya Sh90.2 bilioni kwenye halmashauri 82 nchini ina kasoro.

Hayo yameelezwa leo Jumatatu Oktoba 14, 2019 na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenista Mhagama katika  maadhimisho ya kilele cha mbio za Mwenge mwaka 2019 pamoja na kumbukumbu ya miaka 20 ya kifo cha mwalimu Julius Nyerere.

Amesema Mwenge ulibaini kasoro katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo hasa ya maji, elimu, barabara na ujenzi wa majengo ya umma.

Amesema miradi hiyo haikufunguliwa au kuwekwa mawe ya msingi kutokana na kasoro  hizo zisizoendana na matumizi ya fedha katika miradi husika, kujengwa kinyume na mikataba na makadirio yaliyopitishwa na wataalamu, makandarasi kushindwa kufuata na kusimamia kanuni za ujenzi.

“Ilifanya ubora wa miradi hiyo kutia shaka hususani katika suala la uimara, jambo jingine ni matumizi duni ya vifaa katika miradi ya umma,” amesema.

Amesema umebaini makandarasi kutosimamia majukumu wanayopewa kwa wakati na mamlaka husika na kutokuwachukulia hatua za kisheria.

Amesema baadhi imekuwa na ubora usioridhisha hasa ujenzi wa visima vya juu vya kuhifadhia maji ambavyo kuta zake zilikuwa na nyufa na kabla ya miradi hiyo kuanza kutumika.

“Jambo jingine ni udanganyifu katika lugha za kitaalamu hususani miradi ya maji na ujenzi na hivyo kuwa vigumu kwa viongozi ambao hawana utaalamu kubaini matumizi ya fedha za umma zilizotumika vibaya.”

“Pia, ufanyaji wa makadirio ya gharama za ujenzi zisizoendana na gharama zilizo sokoni,  vitendo vinavyofanywa na wahandisi wetu katika miradi na kuhujumu fedha za watanzania,” amesema Mhagama

Miradi  iliyozinduliwa na kuwekwa mawe ya msingi na Mwenge wa Uhuru nchini ni 1,390 yenye thamani ya Sh4.7 trilioni.