Michepuko chanzo wanaume kuhofia kupima VVU

Muktasari:

Zaidi ya watu 72,000 wanapata maambukizi mapya ya VVU kila mwaka kwa mujibu wa mkurugenzi mtendaji wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS), Dk Leonard Maboko. Asilimia 40 ya wanaoambukizwa ni vijana, hasa wa kike wenye umri kati ya miaka 15 hadi 24.

Mwanza. Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Watu Wanaoishi na Virusi vya Ukimwi (Nacopha), Leticia Kapela amesema tabia ya baadhi ya wanaume kuwa na uhusiano wa mapenzi na wanawake wengi ni moja ya sababu inayowafanya waogope kupima virusi vya Ukimwi.

Akizungumza leo Desemba Mosi, 2019 katika kilele cha siku ya Ukimwi inayofanyika kitaifa jijini Mwanza, Leticia amesema badala ya kupima afya zao, husubiri wake zao kupima afya wanapokuwa wajawazito, wakiona wapo salama nao huamini hawana maambukizi.

"Wapo baadhi ya wanaume wana michepuko inayoweza kujaa mabasi mawili. Hawa hawawezi kwenda kupima VVU kwa kujihofia wenyewe," amesema.

Kuhusu wanawake, amesema baadhi yao ni chanzo cha maambukizi kutokana na kujirahisisha kwa wanaume wanaowataka.

"Mwanamke unashindwaje kusema hapana unapofuatwa na mwanaume,” amesema.

Kaimu meneja wa Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi (NACP), Dk James Kamuga amesema zaidi ya watu milioni 1.6 nchini  wanakadiriwa kuishi na VVU.

Kati yao, zaidi ya 1.2 tayari wameingizwa katika huduma dawa za kufubaza virusi vya Ukimwi zinazotolewa bure na Serikali.