Mipango itakayomaliza uhaba wa madarasa nchini

Changamoto ya uhaba wa madarasa katika shule mbalimbali nchini hasa za Serikali, ni tatizo la muda mrefu linaloikabili sekta ya elimu nchini.

Kila mwaka tunashuhudia idadi kubwa ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na elimu ya sekondari wakishindwa kuanza masomo kwa wakati kutokana na tatizo hilo.

Mwaka jana, Waziri wa Tamisemi, Selemani Jafo alisema kuwa wanafunzi 58,699 waliofaulu kuingia kidato cha kwanza walikosa nafasi kutokana na tatizo hilo. Aliitaja mikoa yenye tatizo hilo na idadi ya wanafunzi kuwa ni Arusha (4,739), Dar es Salaam (5,808), Iringa (3,480), Kigoma (12,092), Lindi (1,695), Manyara (728), Mara (9493), Mbeya (2,716), Pwani (2,918), Rukwa (686), Simiyu (6,616), Songwe (4,684) na Tanga (3,044).

Aliwaagiza viongozi wa mikoa kukamilisha madarasa kabla ya Februari 29, 2020 ili yaanze kutumika Machi 2.

Mwaka 2018, nako wanafunzi 133,747 waliofaulu walikosa nafasi kutokana na uhaba wa madarasa, Waziri Jafo alitoa agizo kwa wakuu wa mikoa yenye tatizo hilo kukamilisha ujenzi wa madarasa ili wanafunzi hao waanze masomo mapema.

Miaka ya nyuma wanafunzi waliokuwa wakikosa nafasi walikuwa wakilazimika kusubiri kukamilika kwa ujenzi wa madarasa, ndipo baadaye waanze masomo, huku wenzao wakiwa wameshaanza kwa zaidi ya mwezi mmoja au zaidi.

Mwaka huu, wanafunzi waliokuwa wamekosa nafasi wamelazimika kuanza masomo wakiwa wamerundikana darasani, baada ya Naibu Waziri wa Tamisemi, Mwita Waitara kueleleza kuwa Serikali imeagiza wanafunzi wote waliofaulu waanze masomo shule zilipofunguliwa jana.

Hali hiyo imekuwa tofauti kwani Desemba 5 mwaka jana, Jafo aliwaagiza wakuu wa mikoa wajenge na kukamilisha madarasa ifikapo Februari 29 mwaka huu, ili wanafunzi hao 58,699 waanze masomo Machi 2.

Hata hivyo, Desemba 29, mwaka jana, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alitoa agizo kwa wakuu wa mikoa nchini kuhakikisha madarasa yanakamilika kwa wakati na wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza waanze masomo kwa pamoja.

Alisema lengo la Serikali ni kuhakikisha wanafunzi wote wanaanza masomo kwa pamoja, kwani wakipishana baadhi yao watashindwa kufanya vizuri.

Pamoja na nia njema ya Serikali, uamuzi huo haukuwa sahihi, kwani unakwenda kinyume na mwongozo wa Serikali unaotaka kila darasa kuwa na wanafunzi wasiozidi 45.

Tatizo hili si la kushtukiza kwa kuwa inafahamika kuwa kila mwaka wanafunzi wanahitimu darasa la saba, hivyo ni muhimu kuwepo na mipango madhubuti ya kulimaliza, ili wanafunzi wasome katika mazingira rafiki na hatimaye ubora wa kiwango cha elimu nchini uongezeke.

Kauli za wadau

Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, Dk Leonard Akwilapo anasema kila mwaka Serikali imekuwa ikitenga bajeti na kujenga madarasa ili kukabiliana na tatizo hilo.

“Mikakati ipo ya kujenga madarasa kila mwaka kwa kuwa tunajua idadi ya watu inaongezeka kila mwaka, hatuwezi kusema watu wasizae,” anasema.

Wakati Dk Akwilapo akitoa kauli hiyo, Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mwita Waitara alisema katika mwaka wa fedha 2018/19, Serikali ilitoa Sh29.9 bilioni kwa ajili ya kukamilisha madarasa 2,392 nchi nzima.

Waitara alikuwa akijibu swali la mbunge wa Lushoto, Shaban Shekilindi bungeni Aprili mwaka jana na kusema kati ya halmashauri zilizopewa fedha hizo, Lushoto ilipewa Sh512.5 milioni kwa ajii ya kukamilisha madarasa 46. Alisema Serikali itaendelea kukarabati na kujenga miundombinu ya elimu kwa awamu kwa kadri ya upatikanaji wa fedha.

Pia alisema katika kipindi hicho Serikali kupitia programu ya ‘Lipa kulingana na matokeo (EP4R)’ ilipeleka Sh467 milioni kwa ajili ya ujenzi wa mabweni, matundu ya vyoo na madarasa katika shule za msingi na sekondari.

Hata hivyo, Waziri Kivuli wa Elimu, Susan Lyimo anasema ni muhimu Serikali kuwa na makisio ya wanafunzi wanaomaliza elimu ya msingi kila mwaka ili ijipange kumaliza tatizo hilo.

Anasema iwapo Serikali kila mwaka itatenga bajeti ya kujenga madarasa na fedha hizo kutumika kwa lengo hilo, tatizo hilo litaisha ndani ya miaka michache.

“Hili tatizo ni la muda mrefu. Mfano mwaka jana (mwaka juzi- 2018) wanafunzi 133,000 waliofaulu walikosa nafasi kutokana na uhaba wa madarasa.

“Hili tatizo linajulikana, sio kila inapofika Desemba, Serikali iwe inatoa matamko kwa wakuu wa mikoa kwamba Januari madarasa yawe yamekamilika. Hivi ni madarasa gani hayo yanayojengwa kwa mambo ya zimamoto?” Anahoji.

Lyimo ambaye pia ni mbunge wa Viti Maalum kwa tiketi ya Chadema, anasema inachofanya Serikali ni kujitoa ufahamu, kwani inafahamu takwimu za wanafunzi na kwamba ingekuwa na mikakati ya muda ya mfupi, wa kati na mrefu tatizo lingeisha.

Anasema kitendo cha wanafunzi kusoma kwa awamu hakina afya, na pia kuhoji walimu watalipwaje kutokana na utaratibu huo.

“Cha muhimu katika kuondokana na tatizo hili ni vema kukawepo na mkakati na mpango maalum kwa kila halmashauri iwe na fungu la kujenga madarasa. Kwa kuwa sasa mapato yote yanakwenda Serikali kuu sasa inabidi itoe fungu kwa kazi hiyo,” anasema.

“Pia Serikali inaweza kushirikiana na wananchi pamoja na uongozi wa shule na kuweka bajeti ya kujenga madarasa. Si sahihi wanafunzi kusubiri madarasa yajengwe, bali madarasa yalipaswa kusubiri wanafunzi. Tukiendelea hivi hakutakuwa na usawa katika elimu,” anasema.

Anasema kuwa kwa wanafunzi 58,699 waliokosa nafasi wakigawanywa kwa wanafunzi 45 kila darasa ni sawa na kusema kunahitajika takriban madarasa 1,300 ambayo anaamini Serikali haishindwi kuyajenga.

“Serikali haishindwi kujenga madarasa hayo ambayo kila moja linagharimu Sh15 milioni kwa kuwa inaweza kununua ndege moja kwa Sh500 bilioni,” anasema.

Anashauri Serikali iwekeze katika elimu ambayo pia itasaidia kutoa wataalamu wazuri na kuisaidia nchi kuondokana na matatizo mbalimbali.

Katika kuunga mkono juhudi za Serikali, Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Deus Seif anasema hivi karibuni walitoa mifuko 300 ya saruji kwa jiji la Dodoma kwa ajili ya ujenzi wa madarasa ya shule za msingi ili kukabiliana na tatizo la uhaba wa madarasa.

“Huu ni mwanzo wa safari yetu ya kusaidia elimu ya Tanzania, CWT tumejipambanua kusaidia kila jitihada za Serikali… tutaendelea kutoa na maeneo mengine yenye uhitaji,” anasema.

Ikumbukwe ubora wa elimu unategemea uwekezaji kwenye rasilimali watu pamoja na miundombinu na vifaa. Elimu bora ni nguzo muhimu katika kumkomboa binadamu kifikra na kiuchumi.

Nchi nyingi zilizofanikiwa kiuchumi duniani, zimewekeza kwenye elimu ya raia wake, hivyo nasi kama taifa ni muhimu kuongeza nguvu katika eneo hilo.