Mke mwingine agomea talaka ya DC kortini

Monday August 5 2019

Mkuu wa Wilaya ya Nchemba aliyevaa suti,Saimon

Mkuu wa Wilaya ya Nchemba aliyevaa suti,Saimon Odunga akitoka kusikiliza kesi yake katika Mahakama ya Mwanzo ya Ukonga 

By Tausi Ally, Mwananchi [email protected] mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Medilina Mbuwuli ambaye ni mke wa ndoa ya Kanisani wa Mkuu wa Wilaya ya Chemba mkoani Dodoma, Simon Odunga amedai katika Mahakama ya Mwanzo ya Ukonga, Dar es Salaam kuwa mumewe huyo hajawahi kutoa matunzo ya mtoto wao wa kike (18) tangu akiwa chekechea hadi sasa yupo kidato cha sita.

Mbuwuli ameieleza hayo leo Jumatatu Agosti 5, 2019 mbele ya Hakimu Christina Luguru ambaye anaisikiliza kesi hiyo ya madai ya talaka namba 181 ya mwaka huu.

Iliyofunguliwa na Odunga.

Hata hivyo ameeleza licha ya mumewe kutotoa matunzo hayo, hayupo tayari kupewa talaka kwa sababu ndoa yao ni takatifu ya Kanisani na kwamba bado anampenda mume wake nna kwamba anajua hizo ni changamoto tu zimempitia.

Katika kesi hiyo, Mbuwuli ameeleza yeye na mumewe tangu wafunge ndoa mwaka 1998 na kupata cheti cha ndoa A no 00140917 hawajawahi kuchuma mali yoyote na hana mgogoro na hilo na kwamba Odunga amechuma mali na kahaba wa nje ya ndoa.

Hata hivyo, amedai katika ndoa yao Odunga amekuwa akikaa kwake akiwa hana fedha na akipata fedha anaishi kwa mwanamke huyo wa nje ya ndoa na kwamba ana mashahidi wa kutosha.

Advertisement

Undani wa kesi hii ya alichokieleza Medilina mahakamani na utetezi wa DC Odunga usikose  gazeti lako la Mwananchi la kesho Jumanne Agosti 6, 2019 utajua  msimamo wa mkuu huyo wa wilaya anayetaka kuwapa talaka wake zake wawili.

Katika kesi nyingine ya madai ya talaka iliyofunguliwa namba 180 ya mwaka 2019 iliyofunguliwa  mahakamani hapo na Odunga dhidi ya ndoa aliyoifunga serikalini  na Ruth Osoro itaendelea kusikilizwa Agosti 19, 2019.

Katika ndoa hiyo inayosikilizwa mbele ya Hakimu Elia Mrema, Odunga anaomba talaka dhidi ya ndoa hiyo ya Serikali aliyoifunga Februari 21, 2010 na Ruth Osoro ambapo walipata cheti cha ndoa B no 0979341.

Analalamikiwa  na mkewe kwa kutokutoa mafunzo ya mtoto wao wa kiume mwenye umri wa miaka minne kwa kipindi cha miaka mitatu.

Licha ya malalamiko hayo, Odunga anaomba mahakamani hapo apewe ridhaa ya kumlea mtoto wao wa huyo wa kiume mwenye umri wa miaka minne bila bughudha yoyote.

Katika kesi hiyo, Odunga anaomba kutoa talaka kwa mkewe huyo  kwa sababu amechoshwa na magomvi na kudhalilishwa sehemu zake za Kazi huku mke  wake huyo akisema amemsamehe mme wake na hayuko tayari kupewa talaka.

Advertisement