Mme, mke kortini tuhuma za uhujumu uchumi, wenzao wasakwa

Muktasari:

Mme na mke ambao ni wakazi wa Salasala jijini Dar es Salaam nchini Tanzania wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakituhumiwa kwa makosa mbalimbali ikiwamo la utakatishaji fedha na uhujumu uchumi.

Dar es Salaaam. Zakayo Mazula (30) akiwa na mke wake Jasmine Ngongolo (30)  wakazi wa Salasala wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam pamoja na wengine wawili ambao hawapo wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu nchini Tanzania wakikabiliwa na mashtaka matano likiwemo la utakatishaji fedha kiasi cha dola za kimarekani 4000.

Akisoma hati ya mashtaka leo Agosti 16,2019 Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi amedai washtakiwa hao wanakabiliwa na kosa la uhujumu uchumi.

Nchimbi amedai katika shtaka la kwanza la kujihusisha na mtandao wa kihalifu ambapo Januari Mosi na Agosti 2, 2019 wote kwa pamoja wakiwa maeneo tofauti jijini Dar es Salaam na Johannesbarg nchini Afrika Kusini walikutwa wakishirikiana na watumishi wa umma kusambaza nyaraka zisizo halali 2,472 za kujazia visa zilizoghushiwa ambazo ni za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Katika shtaka la pili tarehe hiyohiyo wakiwa maeneo hayo kwa pamoja wamepatikana na kosa la kughushi nyaraka za visa 2,472 wakidai hizo ni za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Nchimbi amedai katika shtaka la tatu Agosti 2,2019 katika Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere (JNIA) kwa pamoja walikutwa na nyaraka 2,472 za visa kinyume na sheria ya Jamhuri za Muungano wa Tanzania zilizoandaliwa kwa ajili ya kusafiria.

Shtaka la nne katika tarehe hiyo na maeneo tofauti ya jiji la Dar es Salaam na Johannesbarg washtakiwa kwa pamoja walikutwa wakitengeneza nyaraka hizo za kusafiria bila kuwa na mamlaka ya kufanya hivyo.

Shtaka lingine la utakatishaji wa fedha washtakiwa hao kwa pamoja kati ya Januari Mosi na Agosti wakiwa jijini Dar es Salaam walibadilisha fedha zenye thamani ya dola za Kimarekani 4,000 kwa ajili ya kutumia kujengea nyumba iliyopo maeneo ya Salasala na kufanya matengenezo ya magari matatu kwa lengo la kuficha siri ya fedha hizo huku wakijua ni zalio la uhalifu.

Nchimbi alidai upelelezi bado unaendelea hivyo aliiomba mahakama hiyo itoe hati ya kukamatwa washtakiwa Yusuph Ivere na Kenedy Maleko wakikabiliwa na mashtaka hayo pamoja na la utakatishaji wa fedha dola za Kimarekani 118200.

Inadaiwa kuwa Julai 15, na Agosti 2,2019 katika maeneo ya jiji la Dar es Salaam na mji wa Blantyre uliopo nchini Malawi walijihusisha na miamala ya dola za Kimarekani 118200 kupitia benki ya Stanbic iliyopo tawi la Kariakoo huku wakijua fedha hizo ni zalio la kughushi.

"Washtakiwa Ivere na Maleko wamegundulika kutoroka nje ya nchi mara baada ya kubaini wenzao wamekamatwa hivyo tunaiomba mahakama hii itoe hati ya kuwakamata waweze kufikishwa mahakamani," alidai Nchimbi.

Hakimu Shaidi amesema washtakiwa hao hawaruhusiwi kujibu chochote kwakuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi ya uhujumu uchumi yenye mamlaka ni Mahakama kuu ya Tanzania.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Agosti 30,2019 kusikilizwa tena.