Mongella: Hatutaruhusu mikusanyiko wakati wa pasaka

Friday April 10 2020Mkuu wa Mkao wa Mwanza, John Mongella

Mkuu wa Mkao wa Mwanza, John Mongella 

By Jesse Mikofu, Mwananchi [email protected]

Mwanza. Mkuu wa Mkao wa Mwanza, John Mongella amesema hawataruhusu mikusanyiko ya aina yoyote wakati wa kusherehekea sikukuu ya Pasaka badala yake amewataka watu kusherehekea sikuku hiyo wakiwa nyumbani ili kuepuka ugonjwa wa corona.
Mongella amesema yapo maeneo ambayo kwa asili yamekuwa yakivutia na kuwakusanya watu mbalimbali wakati wa sikukuu za dini au za mwaka kama mwka mpya.
Maeneo hayo ni; daraja la Furahisha, Rocky City Mall, Kemondo, fukwe za Kamanga Ferry na Malaika.
“Niwatakie sikukuu njema yenye amani, na mkoa wetu unahistoria ya kusherehekea sikukuu hizi kwa utulivu na amani, ila kwa kipindi hiki hatutaruhusu mikusanyiko ya aina yoyote kwenye maeneo haya,” amesema Mongella
Amesema ili kuepuka adha na usumbufu utakaojitokeza ni vyema watu wakahakikisha hawatoki nyumbani kukusanyika kwenye maeneo hayo kama ilivyozoeleka badala yake wafurahie kwa pamoja kwenye majumba yao.
Aliwataka kuendelea kujihadhari na ugonjwa wa corona na kuzingatia masharti na miongozo yote inayotolewa na wataalamu ili kuepusha maambukizi mapya ya ugonjwa huo.

Advertisement