Moto waacha madeni, ukata kwa wafanyabiashara Tegeta

Wednesday February 19 2020

Wakazi wa Dar es Salaam wakitazama masalia

Wakazi wa Dar es Salaam wakitazama masalia yaliyobaki kufuatia Soko la Tegeta Nyuki kuteketea kwa moto uliotokea usiku wa kuamkia jana, ambapo jumla ya fremu 14 na vizimba 81 viliteketezwa na moto huo. Picha na Ericky Boniphace 

By Fortune Francis, Mwananchi [email protected]

Dar es salaam. Wafanyabiashara wa soko la Tegeta Nyuki ambalo limeteketea wameeleza namna biashara hiyo ilivyokuwa tegemeo lao kuu na kuiomba Serikali kuwasaidia.

Usiku wa kuamkia jana Februari 18, 2020, moto uliteketeza vibanda zaidi ya 80 na maduka 14 katika soko hilo na hakuna mali iliyookolewa.

Efech Chubwa, mmoja wa wafanyabiashara sokoni hapo, amesema alikuwa na mzigo wa nafaka wenye thamani ya zaidi ya Sh10 milioni ambao umeteketea kabisa.

Anasema alipata taarifa za moto huo saa tano kasoro usiku akiwa nyumbani anajiandaa kulala na alipofika sokoni hapo alikuta moto ukiwa umeteketeza kila kitu.

“Hapa unapoona nina familia ya watoto wanaonitegemea kwa ada na kila kitu, sina la kufanya, baada ya kupata taarifa jana nikiwa nyumbani nilifika na nilipoona hali ilivyo nikarudi nyumbani,” alisema Chubwa.

Mmiliki wa bucha lililokuwa sokoni hapo ambalo limeteketea lote, Issa Issa alisema amepata hasara kubwa kwani tangu afanye matengenezo hata gharama alizotumia zilikuwa hazijarudi.

Advertisement

“Kama unavyojua Desemba ni sikukuu, nilifanya matengenezo na huu ni mwezi wa pili nafanya biashara, hata nusu ya gharama haijarudi. Tunaomba Serikali ituangalie kwa kuwa sisi ndio kila kitu kwenye familia,” alisema.

Naye Salome Mushi, mfanyabiashara mwingine wa nafaka sokoni hapo aliyekuwa akiongea kwa shida kutokana na hasara aliyoipata, alisema hana cha kufanya zaidi ya kuiomba Serikali kuwasaidia.

Alisema hasara aliyoipata ni kubwa sana na hajui atalipaje mkopo kwa kuwa kila kitu kimeteketea na hakuna kilichosalia.

“Kama unavyoona hapa sijaokoa chochote na nimeshusha mzigo siku za karibuni pia nina na mkopo, sina cha kufanya naomba Serikali itusaidie angalau turudi kwenye hali yetu ya kawaida,” alisema Mushi.

Kwa habari zaidi soma gazeti la Mwananchi la leo Jumatano Februari 19,2020

Advertisement