Msanii wa muziki Tanzania afariki dunia

Muktasari:

Ikiwa bado hakuna taarifa kamili kuhusu kifo cha msanii Mbalamwezi wa kundi la The Mafik ndugu zake wamezungumzia taarifa hizo ikiwamo kwenda Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Dar es Salaam nchini Tanzania kupata undani wa kijana wao.

Dar es Salaam. Wakati kukiwa na taarifa za sintofahamu kuhusu kifo cha msanii wa muziki nchini Tanzania, Abdallah Matimbwa maarufu ‘Mbalamwezi’ mjomba wa msanii huyo amesema familia haijui chochote kuhusu kijana wao.

Akizungumza na Mwananchi leo Ijumaa Agosti, 16,2019 mjomba wa Mbalamwezi aliyejitambulisha kwa jina la Chief Mponda amesema taarifa za kifo hicho wamezipata usiku wa kuamkia leo saa nane usiku.

Mponda amesema kwa mara ya mwisho waliwasiliana na Mbalamwezi wiki moja iliyopita na kwa sauti yake alionekana ni mzima wa afya.

 "Tuliwasiliana na Abdallah wiki moja iliyopita aje kumuona mjomba wake mkubwa ambaye anaumwa macho kwa kuwa alikuwa anaishi Kinondoni aliahidi  kufanya hivyo na kuanzia hapo sikuongea naye tena mpaka nilipopata taarifa za kifo chake na kutoka kwa wasanii wenzake," amesema Mponda.

Amesema hata taarifa zenyewe hajazipata kiundani anasubiri waliokwenda Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dar es Salaam kuutambua mwili na kufuatilia mengineyo ili tuelewe nini kimetokea.

Enzi za uhai wake Mbalamwezi akiwa na kundi la The Mafik walitesa na vibao mbalimbali ikiwemo Niwaze waliouimba na Ruby na kuwatambulisha vema kwenye soko la muziki.

Nyimbo nyingine ni Passenger,  Sheba, Bobo, Corola na vuruga waliouachia siku tatu zilizopita.

Endelea kufuatilia Mwananchi kwa taarifa zaidi